Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imepandisha bei za mafuta ya aina zote kuanzia leo isipokuwa Mkoa wa Tanga pekee.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu Felix Ngalamgosi,  jijini Dar es salaam alipokuwa akizungumza kuhusu kupanda kwa bei za mafuta ya jumla na reja reja kwa mafuta ya aina zote.

“Kwa Februari 2017,bei za reja reja zimepanda, petroli imepanda kwa shilingi 69 kwa lita sawa na asilimia 3.64 ambayo ni shil. 1,959, dizeli ni shil.129 kwa lita ambayo ni sawa na asilimia 7.47 ambayo ni sh. 18,61 na mafuta ya taa ni sh.151 kwa lita, sawa na asilimia 8.90,ambayo ni sh.1,852, kwa mkoa wa Dar es salaam,” amesema Ngalamgosi.

Amesema kuwa kulingana na toleo la Januari bei za jumla nazo zimepanda ambapo petroli ni sh.69 kwa lita sawa na asilimia 3.86,dizeli sh.129 kwa lita ambayo ni sawa na asilimia 7.96 na mafuta ya taa ni sh.151 kwa lita sawa na asilimia 9.50.

Amesema kuwa kupanda kwa bei ya mafuta kunatokana na mabadiliko ya bei za mafuta kwenye soko la dunia,kuongezeka kwa gharama za usafirishaji na kushuka kwa thamani ya shilingi dhidi ya dola ya Marekani.

Hata hivyo amesema kuwa hakutakuwa na mabadiliko ya bei za mafuta kwa Mkoa wa Tanga,kutokana na kutopokea mzigo mpya wa mafuta kwenye bandari ya Tanga kwa mwezi Januari.

#HapoKale
Heche ataka fedha za tetemeko zirudi bungeni