Jiji la Dar es Salaam huenda likapata ugeni mzito wa tukio la Tuzo za MTV Africa Music Awards (MAMAs), kama mambo yataenda sawa.

Mwanzilishi wa tuzo hizo, Alex Okisi ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa MTV Networks Africa, alifunguka ‘exclusively’ alipokutana uso kwa macho na mtangazaji wa The Playlist ya 100.5 Times FM, Omary ‘Lil Ommy’ Tambwe kuhusu mpango huo.

Lil Ommy ambaye mwezi uliopita alipiga kambi jijini Johannesburg na kuripoti tukio lote la tuzo za MTV MAMAs 2016, amefunguka katika mahojiano maalum aliyofanya na Dar24 na kusimulia alichoelezwa na Bosi huyo wa MTV Africa kuhusu mpango huo.

“Nilipenda alichokisema… alisema ‘Dar es Salaam ni mji mzuri, ni mji ambao uko sawa na tunajaribu kufanya mikakati na watu wa Serikalini na wadau kwenye industry tuone ni jinsi gani tunaweza kuleta tuzo hizi Tanzania,” Lil Ommy aliiambia Dar24.

“Na jinsi alivyokuwa anaongea ni kama mtu ambaye tayari anajua… kwahiyo nadhani tusubiri tuone,” aliongeza.

Akieleza mtazamo wake kwanini MTV waiwaze Dar es Salaam kama sehemu nzuri ya kufanyia tuzo hizo, Lil Ommy alisema kuwa hii inatokana na jinsi ambavyo Tanzania imekuwa ikizungumziwa vizuri sana kuhusu burudani.

Hata hivyo, mtangazaji huyo alisema anachodhani kinaweza kuliangusha jiji la Dar es Salaam kupata ugeni huo mkubwa ni sehemu ya kufanyia tukio hilo (venue) kutokana na umati alioushuhudia Johannesburg.

“Sina uhakika kama ‘venue’ zetu zina uwezo wa kuchukua watu wengi namna ile (aliyoiona kwenye tuzo za MTV MAMA, Johannesburg). Jamaa wale ni wazuri kwenya maandalizi lakini nadhani tunapaswa pia kuwa na venue ambazo zina viwango vya kimataifa,” alisema.

Angalia mahojiano yote hapa, fahamu kwanini wasanii wa Tanzania kukosa tuzo hizo, kama walionewa au la… na mengine yatakayokufungua:

Wafanyabiashara wa viumbe pori hai wamlilia Rais Magufuli
Tambwe, Mavugo Watemwa Intamba Mu Rugamba