Pamoja na shirikisho la soka nchini TFF kutangaza kuutambua uongozi wa klabu ya Stand Utd FC ulioingia madarakani mwezi uliopita kupitia uchaguzi mkuu, bado upande wa pili wa klabu hiyo (Stand Utd Kampuni) haujafahamishwa kwa njia ya barua kuhusu maamuzi hayo.

TFF kupitia idara yake ya habari na mawasiliano inayoongozwa na Alfred Lucas Mapunda, mwishoni mwa juma lililopita ilitangaza majibu ya kamati ya uchaguzi ambayo ilifunga safari kuelekea mkoani Shinyanga kwa ajili ya kuzungumza na pande mbili zilizokua zinavutana.

Mtendaji mkuu wa Stand Utd Kampuni, Jonas Tiboroha amezungumzia na Dar24.com kwa njia ya simu na kuthibitisha hatua ya kutofahamishwa kuhusu maamuzi hayo, na amesema bado hawajui ni lini watafikishia ujumbe huo kwa njia ya barua.

Amesema wanashangazwa na TFF kushindwa kufanya hivyo ndani ya juma moja tangu walipotangaza maamuzi ambayo kwao wanayaita batili.

“Mpaka leo hatufahamishwa kwa njia ya barua, lakini tunaendelea kuamini maamuzi hayo ni batili kwa sababu hayakuzingatia mambo muhimu ambayo tuliwathibitishia ni nani mwenye haki na klabu ya Stand Utd” Amesema Tiborioha.

Jonas Tiboroha alipokua katibu mkuu wa Young Africans

Kutokana na hatua hiyo, Tiboroha amesema wanajipanga kuwasilisha kesi la kuishitaki TFF katika ofisi za baraza la michezo la taifa BMT, ambapo wanaamini hapo ndipo watakapoipata haki yao ambayo wanadai imeibwa na wasiostahili na kupewa klabu ya Stand Utd.

“Tutawasilisha kesi yetu BMT na huko ndipo tutakapoipata haki yetu kwa sababu TFF ipo chini ya baraza la michezo la taifa kwa kuzingatia sheria za nchi,”

“Hata sisi tupo chini ya BMT kwa hiyo tunaamini tutakwenda kuzungumza na baba wa michezo yote hapa nchini, ambaye amesajili katiba zetu kisheria” Ameongeza Tiboroha.

Kuhusu malalamiko ambayo waliwahi kuyawasilisha FIFA, kuhusu sakata la mgogoro wa Stand Utd, Tiboroha amesema jambo hilo bado lina hatua ya kusikilizwa na shirikisho hilo, kutokana na utaratibu waliojiwekea wasimamizi hao wa mchezo wa soka duniani kote.

“Nimekua na uzoefu na mambo ya FIFA, kama utakumbuka niliwahi kuwa katibu mkuu wa Young Africans na nilishawasilisha malalamiko kuhusu mchezaji Mbuyu Twite, lakini ilichukua zaidi ya miezi mitano ndipo majibu yakatolewa,

“Hivyo hata malalamiko yetu tulioyapeleka FIFA ninaamini majibu yake yatachelewa japo tunaendelea kuwasisitiza waharakishe kusikiliza malalamiko yetu kwa sababu muda unazidi kwenda na ligi inakaribia” ameongeza Tiboroha.

Upande wa Stand Utd kampuni ambao umeshindwa kutambuliwa na TFF unaongozwa na mwenyekiti Aman Vicent ambaye alionekana kuwa mstari wa mbele katika kusaka maendeleo ya klabu hiyo tangu ilipokua ikisaka nafasi ya kushiriki ligi kuu ya soka Tanzania bara msimu wa 2013/14.

Makonda aeleza anapopata kiburi cha kujiita ‘Bingwa wa vita zote’
Joh Makin Afunguka Kuhusu Kumshirikisha Chidnma Perfect Combo