Kocha Mkuu wa Young Africans, Mholanzi Luc Eymael amefurahishwa na taarifa za matarajio ya kurejea kwa Ligi Kuu Tanzania Bara, ambayo ilisimama mwezi Machi kupisha vita dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.

Kocha huyo ambaye kwa sasa yupo nchini kwao Uholanzi, amesema taarifa za matarajio ya kurudi kwa ligi hiyo amezipokea kwa mikono miwili na alikua anatamani iwe hivyo, kutokana na kuamini bado kikosi chake kinahitaji kupambana hadi mwisho wa msimu.

“Kwangu niwapongeze wote wenye mamlaka ya hili, kwani kwa mtazamo wangu wamefanya uamuzi sahihi ambao nina imani wametenga muda wa kutosha mpaka kufikia katika uamuzi huo,” alisema Eymael ambaye anaendelea na mchakato wa kuisuka Young Africans mpya kwa msimu ujao huku wadhamini GSM wakisisitiza hawatanunua mchezaji yeyote wa kukaa benchi.

Awali kocha Luc aliwahi kupendekeza wachezaji wa kila timu wapimwe na kuweka karantini, na wasiruhusiwe kwenda popote, ili kufanikisha mpango wa kuchezwa kwa kwa ligi kuu.

Ligi Kuu ilisimama huku Simba SC ikiwa inaongoza kwa alama zake 71, ikifuatiwa na Azam FC yenye alama 54 baada ya timu zote kucheza mechi 28, wakati vigogo, Yanga SC ni wa tatu kwa alama zao 51 za mechi 27 na Namungo wa nne wakiwa na alama 50 za mechi 28.

Hali ni mbaya kwa Singida United inayoshika mkia kwa alama zake 15 za mechi 29, nyuma ya Mbao FC alama 22 mechi 28, Alliance FC alama 29, mechi 29, Mbeya City alama 30 mechi 29 na Ndanda FC alama 31 mechi 29.

Kabananga: Sijapokea tuzo yangu
Mshauri wa Magufuli awa DC mpya Mtwara