Hamisi Mwinjuma maarufu kama Mwana FA ambaye pia ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), leo amefika katika ofisi za Baraza hilo kuwaombea msamaha WCB.

Juzi, Basata waliwalima WCB adhabu ya Sh. Milioni 9 kutokana na wimbo wa ‘Mwanza’ uliofanywa na Ray Vanny akimshirikisha Diamond Platinumz. Pamoja na adhabu hiyo, Basata waliufungia wimbo huo kutopigwa kwenye vituo vya runinga na redio. Pia, iliwataka WCB kuuondoa wimbo huo kwenye YouTube na kutoutumia katika matamasha yoyote.

Akizingumza muda mfupi baada ya kumaliza kikao na watendaji wa Baraza hilo, Mwana FA amesema kuwa amewaombea msamaha WCB na kwamba anaamini adhabu hiyo itapunguzwa, ingawa sharti la kwanza ni kwa uongozi wa lebo hiyo ya muziki kuandika barua ya kuomba radhi.

“Mimi nilichofanya ni kuwaomba watendaji wa Baraza, kuona hii adhabu tunaweza kufanya nayo nini isiwaumize. Pengine kuna makosa labda yamefanyika lakini tuone namna ambavyo tutawaadhibu bila kuwaumiza,” alisema FA.

“Watendaji wamenielewa na wamesema kwamba uongozi wa Wasafi na wasanii wao wanatakiwa kuandika barua kuomba radhi na kupunguziwa adhabu. Na ninaamini adhabu haitakuwa kama ambavyo imetolewa jana,” aliongeza.

Msanii huyo ambaye ni miongoni mwa wasanii wawili pekee wanaounda Bodi ya Wakurugenzi ya Basata, alisisitiza kuwa alienda kuwaombea msamaha wasanii hao kama mtu binafsi na msanii lakini sio kama mjumbe wa Bodi.

Alisema kuwa Watendaji wa Baraza wana mamlaka ya kutoa adhabu hiyo bila kuingiliwa na mtu yeyote na kwamba suala hilo lingeifikia Bodi endapo tu wasanii walioadhibiwa wangeamua kukata rufaa.

TRC yafufua reli inayounganisha Tanzania na Uganda
Polisi anaswa ‘gesti’ na mwanafunzi anayefanya mitihani

Comments

comments