Mabingwa watetezi wa ligi kuu ya soka nchini England, Chelsea watalazimika kusafiri kuelekea mjini Manchester bila ya kuwa na mlinda mlango wao namba moja Thibaut Courtois, baada ya chama cha soka nchini humo FA, kuiweka kapuni rufaa iliyokua na lengo la kusaka utetezi.

FA wameiweka kapuni rufaa iliyowasilishwa na viongozi wa Chelsea kwa lengo la kumkingia kifua Courtois, kufuatia kadi nyekundu aliyoonyeshwa wakati wa mchezo wa kwanza wa ligi msimu huu baada ya kumchezea hovyo mshambuliaji wa Swansea City, Bafetimbi Gomiz.

Chelsea walikua wanajiamini huenda rufaa yao ingekubaliwa na FA na kufanikisha mpango wa kumtumia tena mlinda mlango huyo kutoka nchini Ubeljigi, kutokana na utetezi waliokua wameuwasilisha lakini mambo yamekua tofauti.

The Blues waliwasilisha utetezi wa kupinga adhabu ya kadi nyekundu kwa Courtois, kwa kuamini Gomiz hakuguswa wakati wa tukio na badala yake alijiangusha kwa makusudi.

Pia The Blues walipandishwa morari kwa kuamini walikua sahihi, kufuatia utetezi uliotolewa na muamuzi mstaafu wa England, Graham Pol kupitia gazeti la Daily Mail la siku ya jumapili, ambapo alipingana na muamuzi wa mchezo kati ya Chelsea na Swansea City, Michael Oliver kwa kudai hakupaswa kumuonyesha kadi nyekundi Courtois.

Kwa mantiki hiyo sasa Chelsea watalazimika kusafiri na kipa chaguo la pili Asmir Begovic, ambaye alishika pahala pa Courtois, mara baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu katika mchezo dhidi ya Swansea city mwishoni mwa juma lililopita.

Mchezo ujao wa utashuhudia The Blues wakisafiri hadi Etihad Stadium kwenda kupambana na Man City ambao juzi walianza vyema msimu wa ligi ya nchini England kwa kuibuka na ushindi wa mabao matatu kwa sifuri dhidi ya West Bromwich Albion.

Chelsea wao walianza ligi kwa sare ya kufungana mabao mawili kwa mawili dhidi ya Swansea City.

Wenje Azungumzia Ujio Mpya Wa Dk. Slaa
Lowassa Atahadharishwa Kuhusu ‘Mafuriko Yake’