Mmiliki wa kampuni ya Facebook, Mark Zuckerberg ambayo inamiliki pia Instagram na WhatsApp, amesema wamefanya mabadiliko makubwa kwenye mitandao hiyo ili kukidhi mahitaji ya watuamiaji.

Amesema kuwa kampuni hiyo imefanya mabadiliko ambayo kwa kiasi kikubwa yamejikita katika kuhakikisha inalinda faragha za watumiaji wa mitandao hiyo, kuweka ulinzi zaidi ili hata wao wasiweze kuona baadhi ya mawasiliano ya watumiaji.

Katika hotuba yake aliyoitoa kwa wataalam wa App hizo, Zuckerberg amsema kuwa katika dunia ya sasa ‘faragha’ ni jambo muhimu na la kwanza.

Ameeleza baadhi ya mabadiliko yanayofanywa kuwa ni pamoja na jumbe zinazotumwa kupitia Facebook Messenger zitakuwa ni ‘end-to-end encrypted’, yaani hata Facebook wenyewe hawatakuwa na uwezo wa kuzisoma, na itaendelea kuwa hivyo pia kwa WhatsApp.

Kwa upande wa Instagram, ameeleza kuwa watumiaji watakuwa na uwezo wa kuficha idadi ya ‘likes’ za kwenye post husika. Yaani mwenye akaunti anaweza kuchagua kuficha idadi ya ‘likes’ za kwenye post husika ili yeye tu awe na uwezo wa kuziona.

Kadhalika, watumiaji wa Instagram watakuwa na uwezo wa kupost jumbe zao hata bila kuweka picha au video, tofauti na ilivyo sasa.

Aidha, kufanya malipo kwa njia ya WhatsApp kama ilivyojaribiwa nchini India, itakuwa inawezekana kwa nchi nyingi zaidi duniani.

“Najua hivi sasa hatuaminiwi sana kuhusu kulinda faragha. Tunapanga kuongeza nguvu zaidi kwenye miundombinu yetu yote, lakini najua haiwezi kutokea kwa usiku mmoja tu,” BBC inamkariri Mark Zuckerberg.

Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Mei 1, 2019
CAG mstaafu awashauri wasioridhishwa na CAG Assad