Mitandao ya Facebook, Instagram, WhatsApp imepotea hewani mapema leo ikiwaacha watumiaji wa mitandao hiyo na sintofahamu. Mitandao yote inamilikiwa na Kampuni ya Facebook.

Taarifa ya kupotea kwa mitandao hiyo imetolewa na msemaji wa Kampuni ya Facebook, Andy Stone  kupitia akaunti yake ya Twitter, akithibitisha kuwa kuna tatizo linalowakabili.

“Tunatambua kuwa baadhi ya watu wanapata shida katika kuingia kwenye mitandao yetu na kupata app na huduma nyingine. Tunafanya kazi kuhakikisha tunarejesha hali ya kawaida haraka iwezekanavyo… na tunaomba radhi kwa usumbufu unaojitokeza,” Stone ameandika.

Hata hivyo, hii sio mara ya kwanza kwa Facebook na mitandao yake mingine kupotea hewani. Aprili na Juni mwaka huu mitandao hiyo ilipotea hewani kwa muda, ambapo ilielezwa kuwa chanzo ni tatizo la mifumo ya mitandao.

Afisa Mkuu wa Teknolojia wa Kampuni ya Facebook, Mike Schroepfer leo ameandika kupitia akaunti yake ya Twitter akiomba radhi.

“Tunaomba radhi kwa kila mmoja aliyeathirika na tatizo la kupotea kwa huduma za Facebook muda huu. Tunapata tatizo la kimtandao na timu yetu inafanya kazi kwa haraka iwezekanavyo kurejesha huduma,” tafsiri ya tweet ya Mike Schroepfer.

Kutokana na hatua hiyo, imebainika kuwa watu wengi duniani wamehamia katika mtandao wa Telegram, kiasi kwamba mtandao huo pia umeanza kufanya kazi kwa kasi ndogo.

Mwanaharakati na mwanasiasa maarufu wa Marekani, Alexandria Ocasio-Cortez ametumia nafasi hiyo kukejeli Facebook akieleza kuwa ni muda mzuri sasa wa kujadili mambo ya maana kupitia mtandao wa Twitter.

Watumiaji wengi wa Twitter wametumia changamoto ya Facebook kutokuwa hewani kuweka kejeli kuwa dunia imerejea kwenye hali yake ya kawaida, kwa madai kuwa Facebook na mitandao yake ya Instagram na WhatsApp husambaza taarifa nyingi za uongo au kupotosha uhalisia.

Nini chanzo:

Ingawa Facebook wenyewe hawajaeleza chanzo, tayari kuna tetesi kadhaa kutoka kwa wataalam na waandishi waliobobea kwenye habari za usalama wa kimtandao, ambao wameeleza kuwa chanzo ni hitilafu kwenye mfumo wa kumbukumbu unaofahamika kama ‘DNS’.

Briankrebs, mwandishi mashuhuri wa Marekani, aliandika kuwa mfumo wa kutunza kumbukumbu wa DNS ambao unakuwezesha kutafuta tovuti za facebook na Instagram ziliondolewa katika uwanda wa dunia.

Facebook kupotea kwaporomosha utajiri wa Zuckerberg ndani ya saa..!
Majaliwa atoa maagizo kwa wakuu wa mikoa