Zikiwa zimebaki siku 21 kukamilisha mzunguko wa kampeni za uchaguzi mkuu nchini, vyama hasimu zaidi vya CCM na Chadema vinatarajiwa kuoneshana ubavu katika fainali ya kampeni hizo, Oktoba 24 mwaka huu huku majiji na Mwanza na Dar es Salaam yakitajwa kuwa maeneo ya matukio.

Duru zinaeleza kuwa, Chadema wamepanga kuhitimisha kampeni zao katika viwanja vya Jangwani Jijini Dar es Salaam siku hiyo, eneo ambalo walifanyia uzinduzi na kufanikiwa kupata gharika zito la watu walioushinda uwanja huo na kuziba barabara zote za jirani.

Wakati Chadema wakiweka wazi eneo lao la tukio, CCM ambao pia wanatarajia kuhitimisha kwa kishindo kizito mbio hizo za kampeni, wamesema kuwa eneo lao la tukio bado ni siri na kwamba muda ukifika wataweka wazi. Mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya CCM, January Makamba alieleza kuwa siku hiyo sio siku ambayo wanaitarajia sana kujihakikishia ushindi kwa kuwa wameshafanya kazi nzuri katika kipindi chote cha kampeni.

“Ng’ombe hanenepeshwi siku ya mnada, hiyo ni siku ya kumalizia tu lakini sio ya kumnenepesha ng’ombe,” alisema January Makamba huku akisisitiza kuwa mgombea wa chama chake yuko vizuri kwa kuwa amefanya kampeni maeneo mengi kwa uhakika.

Hata hivyo, chanzo kililidokeza gazeti la Mwanchi kuwa CCM wanaweza kufanya hitimisho la kampeni zake jijini Mwanza katika uwanja wa CCM Kirumba wanaoumiliki.

Taarifa hizo zinaeleza kuwa, chama hicho pia kinaweza kufunga kampeni zake katika viwanja vya Tanganyika Packers, jijini Dar es Salaam endapo wataona inafaa zaidi kuliko CCM Kirumba, Mwanza.

Mbali na maeneo ya matukio, vyama hivyo vinadaiwa kushindania nafasi ya matangazo ya moja kwa moja ya Televisheni na Radio ili ujumbe wao wa hitimisho uweze kuwafikia watanzania wengi zaidi wakati wanacheza karata yao ya mwisho.

CCM na Chadema walifanya uzinduzi wa kampeni zao katika viwanja vya Jangwani.

Mrisho Mpoto Aeleza Faida Anazopata Kwa Kutembea Peku
Magufuli Awaeleza Ukweli Wana-Singida