Familia ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu aliyeshambuliwa kwa risasi mwezi huu katika eneo la Area D mjini Dodoma, imeeleza kuwa na imani na dereva wake, Simon Bakari aliyekuwa naye wakati wa tukio hilo.

Kaka yake Lissu aliyetajwa kwa jina la Muro Lissu alifanya mahojiano na gazeti la Mwananchi nyumbani kwa baba wa mbunge huyo, Lissu Mughwai katika kijiji cha Mahambe wilaya ya Ikungi mkoani Singida, alisema kuwa kama familia hawana wasiwasi na dereva huyo kwani wanamfahamu kwa zaidi ya miaka 20.

Muro ameeleza kuwa dereva huyo amelelewa na Tundu Lissu tangu akiwa na umri wa miaka 15 alipomtoa nyumbani kwao, kijiji cha Sefuka mkoani humo na kumuendeleza katika fani ya udereva.

“Yule kijana alienda kwa Lissu akiwa mdogo kama kijana wa kazi za nyumbani. Alimchukua katika kijiji cha Sefuka kilichopo Magharibi mwa Singida. Tangu wakati huo alimfunza kazi zote akiwa pale nyumbani kwake. Amemlea, amekulia kwake,” alisema.

“Amekuwa dereva wake tangu alipoanza kuhangaikia jimbo mpaka amechukua ubunge mwaka 2010 na akawania tena 2015 akiwa naye. Wana miaka mingi zaidi ya 20 na yule kijana, amemlea,” Mwananchi linamkariri Muro aliyesisitiza kuwa ni mwanafamilia.

Muro alisema kuwa wakati Lissu anazungumza kuhusu taarifa za kufuatiliwa na wenye gari jeusi, dereva huyo alikuwa anawasiliana na familia ya hiyo na kuelezea mambo hayo.

Jeshi la Polisi linamtaja dereva huyo kama chanzo muhimu cha upelelezi kutokana na kuwepo kwenye tukio na limemtaka kuripoti katika kituo cha polisi.

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ameeleza kuwa dereva huyo yuko jijini Nairobi alipolazwa Lissu na kwamba anapatiwa matibabu ya kisaikolojia.

Video: Rekodi ya Lissu yatikisa kimataifa, Jaji Mkuu abana majaji
Al-shabaab wadai kuhusika na mauji ya Mohamud Qoley