Mahakama nchini Marekani imeamuru familia ya ndugu wa marehemu aliyeuawa na mkuu wa kituo msaidizi kulipwa $4 (sawa Tsh 9,100) kama fidia ya kumpoteza ndugu yao.

Gregory Vaughn Hill Jr, mwenye umri wa miaka 30 alipigwa risasi kupitia mlango wa gereji yake mwaka 2014. Kwa mujibu wa ushahidi wa upelelezi wa polisi uliowasilishwa mahakamani, risasi hizo zilifyatuliwa na mkuu msaidizi wa polisi wa eneo la St Lucie, Florida kufuatia malalamiko ya kelele aliyoyapata.

Jopo la majaji waliosikiliza kesi hiyo lilieleza kuwa kutokana na ushahidi uliowasilishwa na pande zote, hakuna nguvu iliyopita kiasi iliyotumika na kwamba Marehemu Hill anawajibika kwa kifo chake mwenyewe kwakuwa alikuwa amelewa sana.

Jaji aliyekuwa anaongoza jopo hilo aliwauliza wana-jopo wenzake kuamua kama haki ya kikatiba ya Hill ilivunjwa na endapo ni hivyo, waamue kama kuna fidia yoyote inayopaswa kulipwa.

Baada ya saa kadhaa za majadiliano, jopo hilo liliamua kuwa mama wa marehemu anapaswa kulipwa fidia ya $1 kwa ajili ya mazishi na watoto watatu wa marehemu wanapaswa kulipwa $1 kila mmoja, hivyo jumla ya fidia kuwa $4 tu.

Ikieleza sababu za kiasi hicho cha fidia, Mahakama ilieleza kuwa marehemu alijisababishia kifo kwa asilimia 99, hivyo ni asilimia 1 pekee ndiyo inayopaswa kuhesabiwa kosa kwa upande wa pili.

Mchumba wa marehemu alishindwa kuzuia hisia zake nje ya mahakama. “Inapasua moyo, kuna maswali mengi sana natamani kuuliza,” Monique Davis, mchumba wa marehemu anakaririwa na New York Times.

“Nadhani walitaka kuiharibu kesi. Kwanini waamue fidia ya $1? Hiyo inaumiza sana,” alisema mwanasheria wa familia hiyo, John Phillips.

 

Makala: Je unautumiaje urembo wako?
Serikali sasa kutoa ajira ya moja kwa moja kwa wahitimu