Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson amesema kuwa misingi ya utafiti ni jambo muhimu na la msingi litakalopaswa kuzingatiwa katika uchapishaji na utangazaji wa taarifa mbalimbali ili kuweza kulinda misingi ya amani iliyopo nchini.

Ameyasema hayo Jijini Dar es Salaam katika Kongamano maalum la siku ya Amani lililoandaliwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) katika Maonyesho ya 43 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (DITF), ambapo Dkt. Tulia amesema kuwa uchapishaji na utangazaji wa taarifa yoyote haina budi kuwa na tija katika taifa.

Amesema kuwa katika siku za hivi karibuni kumekuwepo na utamaduni uliozoeleka wa kutangaza na kuchapisha taarifa mbalimbali katika jamii kupitia vyombo vya habari pasipo na kuzingatiwa kwa misingi ya utafiti hatua inayoweza kuleta migongano isiyo na tija kwa taifa.

”Serikali ya Awamu ya Tano tunaona inatekeleza miradi mikubwa ya maendeleo, ikiwemo mradi wa umeme katika Mto Rufiji, ni wajibu wetu kulinda misingi ya amani iliyopo ili tuone matunda ya miradi hii katika nchi yetu,” amesema Dkt. Tulia.

Aidha, amesema kuwa ni wajibu wa misingi ya utafiti ikazingtiwa katika taaluma mbalimbali ikiwemo ya uandishi wa habari kwani wapo baadhi ya watu wanaofikiri kuwa wanaweza kuandika na kutangaza habari pasipo na kusomea taaluma hiyo, jambo ambalo si la kweli kwa kuwa uandishi wa habari ni taaluma nyeti na muhimu kama zilivyo taaluma nyingine.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Uandishi wa Habari na Mawasiliano Zanzibar, Imane Duwe amesema kuwa mfumo wa soko huria nchini umeleta mabadiliko makubwa katika tansia ya habari na mawasiliano ikiwemo matumizi ya mitandao ya kijamii, ambayo imekuwa imeleta hamasa kubwa kwa makundi mbalimbali ya kijamii ikiwemo vijana.

Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku amesema kuwa ni wajibu wa Viongozi na Watanzania wajenge utamaduni wa kuheshimu tunu na misingi mikuu ya amani nchini ikiwemo Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, misingi ya Azimio la Arusha ambayo iliasisiwa na Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.

 

Video: TBA yatoa taratibu 4 za kufanya malipo ya nyumba zao
Mbunge atoa angalizo uuzaji wa Mahindi mkoani Njombe