Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO), kwa kushirikiana na Muungano wa Ulaya (EU), limezindua mradi wa kuimarisha Huduma za Afya ya Mimea na usalama wa chakula nchini Tanzania, utakaotekeleza lengo namba 15 la Maendeleo endelevu, kuhusu kuimarisha uhai wa viumbe vya nchi kavu.

Afisa Afya ya Mimea kutoka FAO, Mushobozi Baithani anasema lengo la mradi huo wa miaka mitatu utakaotumia zaidi ya dola milioni 9 sawa na shilingi bilioni 22 za kitanzania, ni kuboresha sekta ya mimea na mazao pamoja na kutatua changamoto kwa wafanyabiashara.

Amesema, “Tanzania wakulima wake wamekuwa wakilima mazao na kusafirisha nje ya nchi lakini zimetokea changamoto kwamba mzigo unafika kule halafu unazuiwa kuingia pengine baada ya kukaguliwa unakutwa na visumbufu, wadudu au umepimwa wamekuta viwango vya viautilifu vilivyowekwa kwenye chakula ni vingi na hakifai kuliwa.”

Aidha, Baithani amefafanua kuwa, “Umoja wa Ulaya umetoa zaidi ya dola mililoni 9 ambazo tutaenda kurekebisha vituo 19 mipakani, tutarekebisha maabara nne, tutanunua vifaaa pamoja na kutengeneza mfumo wa kidigitali utakaotumika kukusanya takwimu mashambani na tumetoa ufadhili wa masomo ya urushaji wa ndege zisizo na rubani kwa wakaguzi 20.”

Naye, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Udhibiti wa Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Efraim Njau amesema, “Mradi huu utatusaidia kufungua masoko kwa sababu tuatenda kulima mazao mapya kama soko la maparachichi, maua, pilipili na tangawizi sasa mazao haya yanafuata huu mfumo.”

Mradi huo pia unatarajia kutoa mafunzo ya kuendesha ndege zisizo na rubani kwa wakaguzi 20, huku Afisa Kilimo kutoka Mamlaka ya Afya ya Mimea na Udhibiti wa Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Masoud Matimbwa akisema hali hiyo itasaidia utafiti na uchunguzi wa wadudu na magonjwa yanayoshambulia mazao ya chakula, biashara na mimea.

Kamanda kundi la waasi akana mashitaka ICC
UN yaondoa hofu tishio la Putin matumizi ya Nyuklia