Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama nchini humo limeweka wazi mshambuliaji aliyeua watu 53 kwenye tamasha la muziki Las Vegas alivyojipanga kutekeleza mauaji hayo.

Imeelezwa kuwa muuaji huyo, Stephen Paddock aliyekuwa na umri wa miaka 64, alikodi chumba kwenye hoteli moja katika eneo ambalo tamasha hilo lilifanyika, siku chache kabla ya tamasha kuanza.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa mshambuliaji alijipanga akiwa na bunduki takribani 19 za kivita ndani ya chumba hicho zenye uwezo wa kurusha risasi mfululizo ndani ya muda mfupi. Pia, alikuwa na vilipuzi kadhaa.

Ndani ya chumba chake, alifunga kamera nyingi ambazo inadaiwa zilikuwa zinamuwezesha kuona watu wanaosogelea chumba chake pamoja na kuangalia nje ya jengo hilo kutafuta eneo analolilenga ambalo ni tamasha lililokuwa na wahudhuriaji zaidi ya 22,000.

Ilipofika Jumapili majira ya saa 4 na dakika 8 usiku kwa saa za Marekani, Paddock alianza kufyatua risasi mfululizo hadi saa 4 na dakika 19. Ndani ya dakika 11 za shambulizi lake akilenga wahudhuriaji bila kuchagua, aliwaua watu 53 na kujeruhi mamia.

Kwa mujibu wa taarifa za polisi, askari wawili wa jeshi hilo ambao hawakuwa kikazi ni miongoni mwa waliouawa kwenye tukio hilo. Paddock alijiua kwa risasi baada ya kutekeleza mauaji hayo.

Ingawa haijafahamika sababu za kutekeleza mauaji hayo, FBI inamshikilia mrembo Marilou Danley ambaye ni  mpenzi wa mshambuliaji huyo kwa ajili ya mahojiano. Danley alikamatwa akiwa jijini Manila nchini Ufilipino na kurejeshwa Marekani.

Msemaji wa kitengo cha uhamiaji  cha Marekani nchini Ufilipino, Maria Antoinette Mangrobang amesema kuwa FBI ilishirikiana na vyombo vya usalama nchini Ufilipino kumpata Danley ambaye wanaamini atakuwa na taarifa muhimu kuhusu mpenzi wake.

Taarifa nyingine zinaeleza kuwa mshambuliaji huyo alituma kiasi cha $100,000 kwa raia wa Ufilipino. Hata hivyo, haikuelezwa wazi kiasi hicho kilitumwa lini na nani hasa alikuwa mpokeaji.

Vyombo vya usalama vya Marekani vinaamini kuwa mshambuliaji alikuwa na sababu binafsi japo hawajabaini hasa ni sababu gani.

Aveva, Kaburu waendelea kusota rumande
Mfalme ahimiza viboko mashuleni!