Beki wa pembeni kutoka nchini Brazil, Daniel Alves da Silva anatarajia kuwa nje ya uwanja kwa muda wa mwezi mmoja, kufuatia majeraha ya nyonga yanayomkabili tangu mwishoni mwa juma lililopita.

Alves alipatwa na maumivu ya nyonga wakati wa mchezo wa ufunguzi wa ligi ya nchini Hispania ambapo FC Barcelona walipambana na Athletic Bilbao na kupata ushindi wa bao moja kwa sifuri mwishoni mwa juma lililopita.

Alves, alishindwa kuendelea na mchezo huo na kutolewa nje katika dakika ya 19 huku nafasi yake ikichukuliwa na Sergi Roberto.

Meneja wa FC Barcelona Luis Enrique amethibitisha kuumia kwa beki huyo mwenye umri wa miaka 32, ambaye amekua msaada mkubwa kwenye kikosi chake.

Enrique, alifanya hivyo kupitia tovuti ya klabu ya FC Barcelona baada ya jopo la madaktari kumfanyia vipimo Alves na kubaini jeraha hilo ambalo litamuweka nje kwa kipindi kirefu.

Wakati Barca wakitarajia kumkosa Alves kwa zaidi ya majuma matatu, timu ya taifa ya Brazil nayo itakosa huduma ya mchezaji huyo katika mchezo wake wa kimataifa wa kirafiki utakaochezwa mwanzoni mwa mwezi ujao.

Benzema Atumia Salamu Kwa Mashabiki Wa Arsenal
Joh Makini Akamilisha Video Na Rapa AKA Wa Afrika Kusini