Mashabiki watakaoshuhudia mchezo wa kirafiki wa mahasimu wa soka nchini Hispania Real Madrid na FC Barcelona watalazimika kulipa Pauni 520, kwa ajili ya tiketi za kuingia uwanjani.

Mahasimu hoa wamepangiwa kukutana Julai 29 katika michuano ya International Champions Cup itakayokuwa na lengo la kuziandaa timu hizo na msimu mpya wa ligi wa 2017/18.

Kiasi hicho cha pesa kitakua ni mara tisa ya kiasi ambacho kitatumika kwa ajili ya kununulia tiketi za mchezo wa fainali wa ligi ya mabingwa barani Ulaya msimu huu, utakaofanyika mjini Cardiff nchini Wales kwenye uwanja wa Millennium.

Tiketi za daraja la chini za mchezo wa fainali ya ligi ya mabingwa zitauzwa Pauni 60, na tayari baadhi ya mashabiki duniani wameripotiwa kuanza kuzinunua, licha ya kutofahamu ni timu zipi zitaitinga fainali.

Kiwango cha juu ambacho kitawahusisha mashabiki wa daraja la kwanza katika mchezo huo wa fainali ya ligi ya mabingwa barani Ulaya, ni Pauni 390, huku mchezo wa El Clasico wa kirafiki tiketi za daraja la kwanza itapatikana kwa Pauni 3600 kwa kila moja.

Mchezo wa El Clasico katika michuano ya International Champions Cup, utakua wa kwanza tangu kuanzishwa kwa michuano hiyo, na umepangwa kuchezwa kwenye uwanja wa Hard Rock nchini Marekani, ambao una uwezo wa kuchukua mashabiki 65,000 walioketi.

Majaliwa awaasa Watanzania waishio nje kutojihusisha na dawa za kulevya
Petr Cech Kukaa Nje Mwezi Mmoja