Uongozi wa mabingwa wa Ujerumani FC Bayern Munich, umemtaka mshambuliaji wao Thomas Muller kuacha kuzungumzia mipango ya usajili ya miamba hiyo ya Bundesliga, kuelekea dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi.

Muller aliiambia timu yake ya Bayern kufuta mpango wa kumsajili mkali wa Bayer Leverkusen, Kai Havertz kwa ada ya Pauni 80 milioni, wakati klabu hiyo ikiwalazimisha wachezaji wake kukubali kukatwa mishahara yao kwa ajili ya janga la Corona.

Muller alisema maneno hayo baada ya Bayern kuibuka na ushindi dhidi ya Eintracht Frankfurt katika nusu fainali ya Kombe la Ujerumani, DFB Pokal.

Mkurugenzi wa Michezo wa Bayern Munich, Hasan Salihamidzic amemwambia mshambuliaji huyo wa Ujerumani afanye yanayomhusu. Havertz pia anasakwa na Manchester United na Chelsea za Ligi Kuu England.

Muller, ambaye pia aliwahi kufukuziwa na Man United, alisema: “Kwa bahati mbaya siwezi kuingia kwenye ile idara ya fedha na ile idara ya mkurugenzi wa michezo. Sifahamu hizi pesa watazitoa wapi kwa wakati huu.

Kuna vitu nashindwa kuvielewa kwenye haya mambo kwa sababu unazungumzia usajili wa pesa nyingi kwa wakati huo unakata watu mishahara yao.”

Bosi Salihamidzic alisema baada ya mechi hiyo alizungumza na Muller na kumweleza kile alichokisema hakikuwa sahihi na hilo.

“Baada ya mchezo, Thomas, aliposhindwa kufurahishwa na kiwango cha uwanjani, aliamua kusema maneno ambayo hayakuwa sahihi. Tulilizungumza hilo siku iliyofuata na nilimweleza hakufanya sawa,” alisema Salihamidzic.

FC Bayern Munich imebakiza ushindi wa mchezo mmoja tu kubeba taji lao la nane mfululizo la Bundesliga.

Ajira: Makampuni 10 yatangaza nafasi za kazi, ziko hapa
Bungeni: Bajeti ya Serikali 2020/21 yapita kwa kishindo