Kiungo wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Feisal Salum Abdallah ‘Fei Toto’ amewaahidi Mashabiki na Wanachama wa Klabu hiyo mambo mazuri katika harakati za kutetea Ubingwa.

Young Africans ina kazi ya kutetea Taji la Ubingwa wa Tanzania Bara msimu huu 2022/23, ikikabiliwa na upinzani mkubwa kutoka Azam FC na Simba SC.

Feisal aliifungia Young Africans bao muhimu na la ushindi Jumapili (Desemba 04), dhidi ya Tanzania Prisons na kuiwezesha klabu hiyo ya Jangwani kurejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu, wakiishusha Simba SC ambayo kwa sasa ipo nafasi ya tatu.

Kiungo huyo kutoka Visiwani Zanzibar amesema kazi yake kubwa iliyompeleka Young Africans ni kuhakikisha Mashabiki na Wanachama wanafurahi wakati wote, hivyo anachokifanya ni sehemu ya kutimiza wajibu wake.

Amesema hatachoka kufanya kazi hiyo pale itakapohitajika, huku akimini hata kwa Wachezaji wenzake watafanya hivyo kwa lengo la kuitetea Young Africans yenye dhamira ya kutete Ubingwa msimu huu.

“Nilisajiliwa Young Africans kwa ajili ya kuwafurahisha Mashabiki na Wanachama wa klabu hii, hivyo inavyotokea mashabiki wakachukizwa na sisi baada ya kupata matokeo mabaya ninaumia sana.”

“Ninawaahidi Mashabiki na Wanachama kuwa nitaendelea kufunga kila nitakapopata nafasi ya kufanya hivyo, ninaamini hata wachezjai wenzangu wana dhamira kama hii ya kuhakikisha tunawafurahisha watu wetu wanaotushabikia usiku na mchana.”

“Ninafahamu upinzani ni mkubwa sana katika Ligi Kuu, jukumu kubwa lililo mbele yetu ni kuhakikisha tunapambana ili kufikia lengo la ushindi ambao tunaupigania kila tunapokua Uwanjani.” amesema Fei Toto

Young Africans leo Jumatano (Desemba 07), itacheza mchezo wake wa 15 wa Ligi Kuu msimu huu, dhidi ya Namungo FC katika Uwanja wa Majaliwa mjini Ruangwa mkoani Lindi.

Jumuiya ya Kimataifa yalaumiwa mgogoro wa DRC
Simba SC yafunguka usajili wa Ntibazonkiza