Uongozi wa Klabu Bingwa Tanzania Bara Young Africans umesema Kiungo kutoka visiwani Zanzibar Feisal Salum Abdallah ‘Fei Toto’ atakabidhiwa medali yake ya ushindi wa Ligi Kuu Tanzania Bara na endapo itabeba ubingwa wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika atapewa pia.

Mwanasheria wa klabu hiyo, Simon Patrick amesema wanatambua Fei Toto ni mchezaji wao halali hivyo ni haki yake kama wachezaji wengine kupata medali ya ubingwa wowote utakaochukuliwa na klabu.

“Medali yake ya ubingwa Ligi Kuu ipo na atapata pia kama tutachukua Shirikisho Afrika atapata medali pia,” amesema Patrick.

Tayari Young Africans imeshanyakua ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara lakini bado wana nafasi ya kushinda ubingwa wa Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC; baada ya kuichapa 0-1 Singida Big Stars, katika mchezo wa Nusu Fainali uliopigwa jana Jumapili (Mei 21) katika Uwanja wa CCM Liti mkoani Singida

Young Africans pia wanaweza kushinda ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Soka Barani Afrika  watakapocheza Fainali dhidi ya USMA ya Algeria Mei 28 na Juni 3.

Kiungo huyo hajaichezea Young Africans tangu Desemba mwaka jana baada ya kuomba kuvunja mkataba na kuilipa klabu hiyo gharama za mkataba wake.

Hata hivyo, ombi lake lilikataliwa na licha ya kukata rufaa kwenye Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’ pia aligonga mwamba kwa rufaa zake kutupiliwa mbali.

Mkataba wa mchezaji huyo na Young Africans unatarajiwa kufika tamati Mei 30, 2024.

Xavi akataa kuilaumu, kuicheka Real Madrid
Magonjwa ya mlipuko: Elimu ya afya ni muhimu kwa jamii