Aliyekua beki wa timu ya taifa ya England na klabu ya Manchester United Rio Ferdinand, amesikitishwa na kitendo cha kunyimwa leseni ya kuwa bondia wa ngumi za kulipwa duniani.

Ferdinand mwenye umri wa miaka 39, alitangaza kustaafu soka mwaka 2015, na kugeukia upande wa masumbwi kwa kuamini ana uwezo wa kupambana katika tasnia hiyo, kama alivyokua akifanya kwenye soka.

Mwaka 2017 mwezi Septemba, alitangaza rasmi kuingia katika ulimwengu wa masumbwi ya kulipwa na tayari alishawahi kuweka picha katika mitandao ya kijamii zikimuonyesha akiwa katika mazoezi ya ndondi.

Bodi ya ngumi za kulipwa nchini England (BBBofC) kimethibitisha kupokea maombi ya Ferdinand, lakini ikasisitiza kutompatia leseni kama alivyokua akitarajia, baada ya kubaini anakosa baadhi ya sifa.

Baada ya majibu hayo, Ferdinand amesema amefadhaika kuona ombi lake limekataliwa na hakutarajia kama mambo yangefikia hatua hiyo na kumkatisha tamaa katika ndoto zake.

“Nilikua na matarajio makubwa ya kuwa bondia mahiri duniani, nimesikitika sana kupata jibu tofauti kutoka kwenye bodi ya kusimamia mchezo wa masumbwi,” Amesema Ferdinand.

“BBBofC walipaswa kunipa angalau nafasi ya kutimiza ndoto yangu ya kuwa bondia wa kulipwa duniani, ili nionyeshe uwezo wangu ulingoni, lakini kama wameamua kutonipa leseni, sina budi kutafuta mbinu nyingine, ila nimeumizwa sana.”

Tayari Ferdinand alikua ameshaanza kupewa ushirikiano na kampuni ya kubashiri matokeo ya michezo ulimwenguni ya Betfair, na ilikua ni moja ya hatua kubwa alioipiga tangu alipotangaza kuingia kwenye mchezo wa masumbwi.

Kocha anaemnoa Ferdinand aliepata mafanikio ya kutwaa ubingwa wa ligi ya soka England mara sita, ni Richie Woodhall ambaye aliwahi kuwa bingwa wa uzani wa kati duniani kuputia mkanda wa WBC.

Mohamed Salah: Sistahili kulinganishwa na Ronaldo
Wizara ya Habari yafungua milango kwa wanahabari