Miaka kadhaa iliyopita, wasanii wote nchini walilazimika kuwasilisha albam zao kwa wasambazaji wenye asili ya kigeni waliobatizwa jina la ‘Wadosi’, kabla ya kusikika kelele za kuibiwa na baadae biashara hiyo kutoswa.

Kufuatia mkasa huo, Fid Q ambaye ni mmoja kati ya wasanii waliofanya biashara na mdosi kupitia albam yake ya ‘Propaganda’, ameiambia Ladha 3600 ya E-FM kuwa alishuhudia jinsi ambavyo msambazaji huyo alivyokuwa akimuibia mauzo na kwenda kinyume na makubaliano.

Fid Q alieleza kuwa kuna wakati Mdosi alimwambia kuwa nakala za albam yake zimekwisha hivyo wanapaswa kugonga nakala nyingine, lakini bahati mbaya makubaliano yao hayakwenda sawa kwa kutokubaliana kimaslahi hivyo hakuna nakala mpya iliyosainiwa.

Alisema kuwa ingawa mdosi aligoma kusaini mkataba mpya, msanii huyo alipopata safari ya nje na akajaribu kununua nakala za albam yake, alijikuta akipata nakala za kutosha kwa Mdosi huyo wakati aliambiwa awali zimekwisha.

“Baada yaa kugoma… si ilibidi mzigo uwe umeshakwisha kwake kama alivyosema ameshauza wote. Mimi nikapata safari baada ya mwezi kwenda nje, unajua mimi nikienda nje huwa napita kwa mhindi nanunua CD zangu mwenyewe kwa bei ya jumla,” alisema.

“Cha kuchekesha, kila nikienda nikiuliza nakala napata za kutosha tu na wakati alinambia mzigo umeshaisha [na hatujagonga nakala nyingine],” alifunguka.

Hii ilimaanisha kuwa Mdosi alikuwa akichapisha nakala za ziada za albam za wasanii kinyamela na kuziuza bila wasanii husika kupata kitu.

Ngosha aliongeza kuwa hata kabla ya albam hiyo, aliwahi kushindwana na mdosi huyo na kuamua kuwa maskini jeuri kwa kutompa CD ya albam hiyo baada ya kutokubaliana kimaslahi. Rapa huyo aliamua kubaki na makasha ya albam yake kuliko kufanya biashara na mdosi isiyo na maslahi.

“Ile albam [Vina Mwanzo, Kati na Mwisho] jamaa alinambia nitoe CD.  Idadi ya CD aliyonipa mimi niliikataa. Kwahiyo mimi nikabaki na makava ya CD nyumbani, mpaka leo ninayo,” Fid aliiambia Ladha 3600.

Hata hivyo, rapa huyo ameeleza kuwa hadi sasa kuna soko kubwa la albam nchini lakini mashabiki hawajui ni jinsi gani wanaweza kuzipata kazi halisi za wasanii. Hivyo, endapo kutakuwa na utaratibu mzuri, wasanii watafanya biashara nzuri ya albam.

Mkali huyo wa mashairi na ‘flow’, alisema mfumo wa ununuaji wa albam kwa njia ya mtandao bado haujawa rafiki kwa soko la Tanzania.

TB Joshua avunja ukimya kuhusu utabiri wake kuwa Clinton angeshinda Urais
Video: Tetemeko kubwa latokea New Zealand