Gumzo lililoibuka kwenye mitandao ya kijamii wiki hii kuhusu kukosekana kwa wasanii wa Hip Hop Tanzania kwenye tuzo mbalimbali za kimataifa, umevuta usikivu wa Fid Q ambaye ni mmoja kati ya wana Hip Hop waliojenga ngome kubwa ya mashabiki ndani na nje ya nchi.

Fid ambaye anahesabu siku kadhaa kabla ya kuachia albam yake ya ‘Kitaaolojia’, Agosti 13 ambayo ni kumbukizi ya siku yake ya kuzaliwa, amesema kuwa anaamini hakuna Afrika nzima hakuna Nchi yenye wasanii wengi ambao pia ni wakali kwenye Hip Hop kama Tanzania.

Tweet ya rapa huyo anayefahamika pia kama ‘Ngosha’, ilikuwa na ujumbe mwingine unaoweza kutafsiriwa kuwa kuna mkondo wa ‘washika dau’ ambao ni chanzo cha tatizo kutokana na wao kuwa na hali nzuri ya kimaisha huku wakiwavuta shati wasanii wenye njaa ya kufanikiwa.

Baadhi ya mashabiki wametoa maoni yao huku wengi wakisema kuwa wasanii wengi hawana nidhamu kwa sanaa wanayoifanya.

“Kuna miungu watu na pia siku hizi kuna wasanii wana majina sana na wanasifiwa sana na WADAU but nna uhakikia after peak yao fake kuisha tutaanza kujadili kuwa walidhurumiwa kumbe walisaini mikataba ya Karl Peters na Chief Mangungo wa Msovero,” aliandika mtumiaji wa Twitter, Hamzalbhanj.

Hata hivyo, baadhi walieleza kuwa endapo wasanii wa Tanzania wakiendelea kufanya kazi nzuri, ipo siku milango itafunguka.

”HipHop haitegemei video kali, Audio ikiwa kali tuu kila kitu kingewezekana naamini kwenye sentesi ya mwisho ya Fid kuhusu ukiritimba hapa bongo ndo chanzo cha rap game kudorora,” aliandika shabiki mwingine.

Hivi karibuni, kumekuwa na mfululizo wa tuzo zinazotolewa Afrika lakini majina ya wsanii wa Tanzania, wa Hip Hop na hata Bongo Fleva yamekuwa adimu tofauti na ilivyokuwa miaka miwili iliyopita.

 

 

Lissu ajipanga na vielelezo 27 mahakamani kudai ubunge
Video: Dkt. Bashiru Ally amtaka Waziri Mkuu kusimamia watendaji