Ushindani uliogeuka kuwa uhasama wa wazi kwenye familia ya biashara ya Mzee Joseph Kusaga, umezaa mkwaruzano wa aina yake kati ya baadhi ya wasanii na waandaaji, na Fid Q amekuwa muathirika.

Kusaga ambaye ni mmiliki wa Clouds Media Group ambao ni waandaaji wa tamasha la Fiesta, ndiye mmiliki/muwezeshaji wa Wasafi inayoandaa ‘Wasafi Festival’. Waandaaji wa matamasha haya wamezua uhasama ulioanza kama ushindani.

Msanii huyo kutoka Mwanza, jana alijibu makombora ya wazi aliyorushiwa na Meneja wa WCB, Babu Tale kupitia mitandao ya kijamii, baada ya kuona kipande cha video cha tangazo la Fiesta ambacho Fid alisikika akirusha jiwe gizani kwa ‘anayesubiri Fiesta wafanye apime ndipo afanye yeye’. Maneno ambayo baadhi ya watu akiwemo Babu Tale waliyachukulia kama yanailenga Wasafi.

Fid aliandika ujumbe mrefu kwenye Instagram, pamoja na mambo mengine, alikumbushia wakati ambapo aliwahi kuwa na matatizo na Clouds Media Group inayojulikana kwa lugha ya mtaani pia kama ‘Mjengoni’, kama ambavyo wasanii na uongozi wa WCB walivyo.

Mkali huyo wa mashairi na mitiririko alimueleza Babu Tale kuwa wakati huo, alipambana mwenyewe na hakuna aliyemsaidia na kwamba alijifunza jambo kutokana na mapambano hayo.

“Kumbukeni mimi pia nishawahi kuwa na matatizo na MJENGO.. lakini nilijikuta ninapambana peke yangu hadi UTULIVU uliporejea pasina msaada wa mtu yeyote.. na sikupambana peke yangu kwasababu hamkua na taarifa, taarifa mlikua nazo lakini ninafikiri mlikua mmetingwa na shughuli zenu za ujenzi wa taifa kiasi kwamba hamkuona kama kuniongezea nguvu ingesaidia lile zoezi kuisha haraka.. amini msiamini sijawahi kumuwekea mtu yeyote kinyongo kwenye hilo, na hiyo kitu ilinifunza sana juu ya suala zima la KUJIPAMBANIA MIE MWENYEWE kwenye situation yoyote ile na KUTOKUPIGANA VITA NISIYOIJUA au ISIYONIHUSU,” inasomeka sehemu ya ujumbe wa Fid.

Aidha, Fid aligusia jambo lingine linaloashiria kuwa Batu Tale alitaka kumshawishi asifanye kazi ya Fiesta na badala yake afanye Wasafi.

“Sioni ni busara kwa nyie kuja na kujaribu kunipangia yupi nifanye nae au yupi nisifanye nae ili kuwaridhisha machoni/ mioyoni mwenu… na kama mnaamini ni haki yenu ya msingi mimi kuyafuata hayo matakwa yenu basi naomba nikujuzeni ndugu zangu mtakua mmeonyesha UBINAFSI wa hali ya juu kwenye hili,” ameeleza.

Kabla hajaomba radhi, Ngosha pia ameeleza kuwa amejifunza kutoingilia vita ambayo haifahamu kutokana na mapito aliyoyapita kwenye migororo ya maisha ya muziki na kwamba hana kinyongo na mtu yeyote.

Fid alikamiliza kwa kumomba radhi Batu Tale na wote waliokwaza kutokana na kauli yake kwenye tangazo hilo la Fiesta ya Dar es Salaam.

“Naomba mnisamehe kibinadamu kwa hilo ,naomba tumuache SHETANI apite na mwisho naomba nimalize kwa kusema.. BURUDANI sio VITA <hivyo ninawatakia kila la heri/ MAFANIKIO ya hali ya juu ktk MAPINDUZI YA BURUDANI huko MTWARA.. KEKI YA TAIFA NI KUBWA SANA NA INA VIPANDE VINGI VINAVYOTOSHA KUMFIKIA KILA ANAYESTAHIKI KWA KUDRA ZAKE MUWEZA WA VYOTE…. MAULID NJEMA,” aliandika.

Maelezo ya Fid Q ambayo aliyaita ‘kigazeti’, yalitokana na video zilizowekwa kwenye Instagram na Babu Tale akiwa n Said Fella, ambao walionekana kumkejeli Fid Q, wakidai hajafanikiwa hata kununua ‘kigari’, na wakienda mbali zaidi kutumia lugha zenye ukakasi kuhusu ngozi ya uso wake na maisha yake binafsi.

Tamasha la Fiesta litahitimishwa Novemba 24 jijini Dar es Salaam, siku ambayo tamasha la Wasafi litakuwa linafanyika kwa mara ya kwanza Mtwara.

Neymar, Mbappe waiweka njia panda PSG
Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Novemba 21, 2018