Shirikisho la soka duniani FIFA hii leo litampta kiongozi mpya, kufuatia uchaguzi mkuu wa rais ambao utaamuliwa na wajumbe 207 waliofika mjini Zurich, Uswiz tayari kwa zoezi hilo ambalo litahitimisha safari ya uongozi wa aliyekua rais kwa kipindi cha zaidi miaka 15 Sepp Blatter.

Blatter, mwenye umri wa miaka 79, aliongoza shirikisho hilo tangu 1998.

Aling’atuka mwaka jana kutokana na tuhuma za ufisadi zilizogubika shirikisho hilo.

Katika kinyang’anyiro cha kuwania nafasi ya urais, FIFA ina wagombea ambao wameweka dhamira ya kumrithi mzee huyo kutoka nchini Uswiz.

Wagombe hao ni Sheikh Salman bin Ebrahim al-Khalifa, Gianni Infantino, Mwana mfalme Ali bin al-Hussein, Tokyo Sexwale na Jerome Champagne.

Sheikh Salman na Gianni Infantino ndio wanaopigiwa upatu kushinda.

Upigaji kura utaanza saa 12:00 GMT (saa tisa alasiri saa za Afrika Mashariki).

Kabla ya kura kupigwa, kila mgombea atakuwa na dakika 15 za kuhutubia wajumbe.

Kuna mataifa 209 wanachama wa FIFA lakini Kuwait na Indonesia kwa sasa hawashirikishwi, hivyo wajumbe watakaopiga kura ni 207.

Ili kutangazwa mshindi duru ya kwanza, mgombea anahitaji kupata theluthi mbili ya kura zilizopigwa.

Hili lisipofanyika, wagombea wote wanapigiwa kura tena duru ya pili na anayepata kura nyingi kutangazwa mshindi.

Mshindi akikosekana duru ya pili, basi duru ya tatu hufanyika bila mgombea mwenye kura chache zaidi raundi ya pili.

Fifa imesema lazima mshindi ajulikane leo Ijumaa.

 

Rais Wa Nigeria Atimiza Ahadi Baada Ya Miaka 30
Marekani yakumbwa na majonzi tena, raia wauawa na kujeruhiwa