Shirikisho la Soka Duniani ‘FIFA’ limewapitisha wagombea wote wanne kugombea katika uchaguzi Mkuu wa Rais wa Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ uliopangwa kufanyika tarehe 12 Machi 2021 mjini Rabat, nchini Morocco.

Wagombea hao ni Augustin Senghor (Senegal), Jacques Anouma (Ivory Coast), Ahmad Ould Yahya (Mauritania) na Patrice Tlhopane Motsepe (Afrika Kusini).

Patrice Motsepe na Ahmed Yahya, nao wamepitishwa ili kuwania urais wa CAF licha ya mashaka ya hapo awali juu ya ustahiki wao.

Kamati ya Marekebisho ya FIFA imesema wagombea wote nne wanaweza kushindana Kwenye uchaguzi wa Machi 12, hivyo Patrice Motsepe na Ahmed Yahya watachuana na Jacques Anouma na rais wa Chama Cha Soka Senegal, Augustin Senghor.

Mnamo Januari 8, taarifa ya CAF ilieleza “ukaguzi zaidi ulikuwa muhimu kabla ya uamuzi wa mwisho” juu ya Motsepe, mmiliki bilionea wa Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, na Yahya, ambaye ameliongoza Shirikisho la Soka nchini Mauritania tangu 2011.

Siku moja baadae, rais wa muda wa CAF, Constant Omari aliandaa kikao cha kamati ya dharura ambapo ilielezwa kuwa FIFA itaamua ustahiki wa wagombea na sasa FIFA imesema wote wapo Safi kugombea.

Aliyekuwa Rais wa CAF Ahmad Ahmad, ambaye alikuwa na matumaini ya kuwania muhula wa pili kama rais wa CAF hadi alipopigwa marufuku na FIFA mnamo Novemba, ameonekana kuwa hana haki ya kushiriki katika uchaguzi huo.

Mdau huyo wa soka kutoka nchini Madagascar, tayari ameshakata rufaa katika Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo ‘CAS’ lakini hadi kutangazwa kwa hukumu, uchaguzi mkuu wa CAF utakua umeshafanyika.

Ngoma arithi mikoba ya Chikwende
Watakao pandisha bei ya mafuta ya kula kufutiwa leseni