Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) imeifungia klabu ya Ligi Kuu ya NBC ya Biashara United ya Mara kusajili wachezaji kwa madirisha mawili.

Adhabu hiyo imetolewa baada ya Biashara United kushindwa kuheshimu uamuzi wa awali wa FIFA kuifungia kusajili wachezaji hadi itakapokamilisha malipo ya madai ya mishahara ya aliyekuwa mchezaji wake Timoth Balton Omwenga.

Kutokana na kutoheshimu uamuzi huo, ndipo FIFA ilipowasilisha suala hilo katika Kamati yake ya Nidhamu ambayo Mei 19, 2022 ilitoa adhabu hiyo kupitia kwa Mjumbe wake Carlos Teran wa Venezuela.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linazikumbusha klabu kuheshimu mikataba ambayo zinaingia na wachezaji pamoja na makocha, kwani hiyo ni moja ya vigezo vya kupata Leseni ikiwa ni utekelezaji wa Kanuni ya Leseni za Klabu (Club Licensing Regulations).

Wajane waomba sheria za mirathi zifanyiwe mabadiliko
Mapitio gharama za matibabu ya figo kuangaliwa upya