Mshambuliaji kutoka DR Congo Fiston Mayele amesema hajabahatika kuwa mfungaji bora msimu huu, kutokana na ukosefu wa umakini wa mwamuzi.

Mayele alihitaji bao moja kwenye mchezo wa mwisho dhidi ya Mtibwa Sugar, ili kutwaa kiatu cha dhahabu kwa misingi ya kanuni za Ligi Kuu msimu wa 2021/22.

Mshambuliaji huyo amesema ana uhakika bao alilofunga dakika za mwisho lilikua halali, lakini maamuzi ya kudhaniwa alikua ameotea yamemnyima nafasi ya kufikia lengo lake msimu huu.

“Nina uhakika lilikuwa bao halali, sikuwa nimeotea, lakini ninaheshimu maamuzi yaliyochukuliwa dhidi yangu na kukubali nimeshindwa kufikia lengo langu.”

“Nilidhamiria kuwa mfungaji bora katika msimu wangu wa kwanza hapa Tanzania, baada ya kuisaidia timu kutwaa ubingwa, lakini sasa ninajipanga kwa msimu ujao, nina uhakika nitapambana na kufikia lengo.” amesema Mayele

Mshanbuliaji huyo aliyejiunga na Young Africans mwanzoni mwa msimu huu akitokea AS Vita, amefanikiwa kufunga mabao 16 ya Ligi Kuu, akitanguliwa na Mshambuliaji mzawa wa Geita Gold George Mpole, aliyemaliza msimu kwa kufunga mabao 17.

Habari kuu kwenye magazeti ya leo Juni 30, 2022   
Maagizo Aweso bili za maji