Mshambuliaji wa Young Africans Fiston Kalala Mayele, amewatumia salamu KMC FC kuelekea mchezo wa mzunguuko wa tatu wa Ligi Kuu Tanzania Bara, utakaopigwa kesho Jumanne (Oktoba 19), Uwanja wa Majimaji mjini Songea, mkoani Ruvuma.

Katika mchezo huo Young Africans itakua ugenini, kufuatia KMC FC kuuchagua Uwanja wa Majimaji kwa mujibu wa kanuni za Ligi Kuu msimu huu 2021/22, ambapo klabu shiriki ina uhuru wa kuchagua Uwanja wowote nchini kwa michezo isiyopungua miwili.

Mayele ambaye anatarajiwa kuwa sehemu ya koksi cha Young Africans kitakachoikabili KMC FC kesho Jumanne (Oktoba 19), amesema utakuwa mchezo ngumu kwa sababu wapinzani wao wataingia kwa nia ya kuwazuia, lakini ana uhakika wataibuka na ushindi kwa sababu wamedhamiria msimu huu kila mechi kuondoka na alama tatu.

“Tunakwenda kucheza na KMC, tunajua kuwa utakuwa mchezo ngumu, sisi kwetu michezo yote zote tunataka alama tatu. Najua Fiston atafanya kazi yake kama kawaida, atakuwa akishirikiana na wenzake, basi hakuna kitakachoshindikana, mechi zote tunahitaji ushindi,” amesema mshambuliaji huyo aliyesajiliwa akitokea AS Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ingawa mpaka sasa hajafunga kwenye mchezo wowote wa Ligi Kuu.

Young Africans imeshacheza michezo miwili ya Ligi Kuu msimu huu 2021/22 dhidi ya Kagera Sugar na Geita Gold FC na imeshinda bao 1-0 katika kila mchezo, huku ikijikusanyia alama 06.

KMC FC ambao watakua wenyeji katika mchezo wa kesho Jumanne (Oktoba 19) Uwanja wa Maji Maji, imecheza michezo miwili, ikipoteza dhidi ya Polisi Tanzania kwa mabao 2-0 kisha iliambulia sare ya 0-0 dhidi ya Coastal Union.

Tuchel: Mendy anastahili heshima
Simulizi:Ushuhuda wa Mchungaji kuhusu kupata waumini watiifu.