Mshambuliaji kinara wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Fiston Kalala Mayele, amewaita Mashabiki na Wanachama wa Klabu hiyo, Uwanja wa Benjamin Mkapa ili kuipa nguvu timu yao.

Young Africans itacheza jijini Dar es salaam baadae leo Jumatatu (Januari 23) dhidi ya Ruvu Shooting inayonolewa na Kocha Mzawa Mbwana Makata.

Mayele amesema anatamani kuona kikosi chao kikiwa na nguvu ya Mashabiki ambao mara zote wamekua msaada mkubwa kwao kama wachezaji.

“Kama kawaida malengo yetu ni kuhakikisha kuwa katika kila mchezo tunaibuka na ushindi, hata mchezo dhidi ya Ruvu Shooting matarajio yetu ni kuona tunapata ushindi mzuri ili tuendelee kuongoza Ligi.”

“Kwa upande wangu binafsi natamani kuona kuwa ninaendelea kufunga mabao muhimu ili niendelee kuisaidia timu, naamini kila kitu kinawezekana hivyo mashabiki wa Young Africans wanatakiwa kuja kutupa nguvu ya kupambana.” amesema Mayele

Young Africans inaendelea kuongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikifikisha alama 53 baada ya kucheza michezo 20, huku Simba SC iliyocheza michezo 21 ikifuatia nafasi ya pili kwa kumiliki alama 50.

Ruvu Shooting itakayopambana na Young Africans inaburuza mkia kwa kuwa na alama 14, baada ya kucheza michezo 20.

Brazil, Argentina zakusudia kuwa na sarafu moja
Afya Day: Chupa 100 za damu zakusanywa SJUT