Mshambuliaji Kinda wa Klabu ya Arsenal Folarin Balogun ni kama amegoma kurudi kwa Washinka Bunduki Wa London, baada ya kubainisha kuwa hajui lolote kuhusiana na maisha yake ya baadae baada ya kumaliza mkataba wake wa mkopo na klabu ya Reims ya Ufaransa.

Balogun amekuwa na kiwango cha juu ndani ya Reims inayoshiriki Ligi Kuu Ufaransa ‘Ligue 1’ na hadi sasa ameifungia timu hiyo mabao 17 katika michezo 27 za msimu huu akicheza ndani ya timu hiyo kwa mkopo wa msimu mmoja.

Kiwango hicho kimekuwa kikizishawishi baadhi ya Klabu kubwa Barani Ulaya kujaribu kumsajili Mshambuliaji huyo ikiwemo AC Milan ya Italia.

Akizungumzia juu ya mustakabali wake, Balogun mwenye umri wa miaka 21, amesema: “Ndiyo, ninamaanisha kimkataba ni lazima lazima nirudi. Kwa sababu ni mkataba wa mwaka mmoja na hayo ndiyo yalikuwa makubaliano.”

“Lakini sipo tayari, sina hakika kama hilo linaweza kutokea huko mbele. Vitu vingi vinatokea kwenye soka, vitu vingi vinabadilika na itategemea na mazungumzo baina ya mimi na klabu mwisho wa msimu na hapo tutaona nini kitatokea.”

“Nimekuwa na msimu bora hapa (Ufaransa) na ninaweza kubakia hapa kwa kuwa kuna kundi kubwa la watu ambao wananifanya niendelee kuwepo hapa na milango haijafungwa.”

Ilkay Gundogan amnyima usingizi Xavi
Morrison kuikabili Simba SC Ligi Kuu