Mshambuliaji wa pembeni kutoka nchini Ufaransa na klabu ya  Bayern Munich Franck Ribery, amesaini mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia The Bavarians.

Ribery mwenye umri wa miaka 35, amesaini mkataba mpya na FC Bayern Munich ambao utamuwezesha kuendelea kuitumikia klabu hiyo hadi mwishoni mwa msimu ujao.

Mkataba wa sasa wa mshambuliaji huyo aliejiunga na FC Bayern Munich akitokea Olympique de Marseille ya nchini kwao Ufaransa mwaka 2007, ulikua unafikia kikomo mwishoni mwa msimu huu, ambao umeshuhudia akifunga mabao matano katika michezo 19 aliocheza.

“Tunayo furaha kuwajulisha kwamba, Franck ataendelea kuwa nasi kwa msimu mmoja zaidi,” imeeleza taarifa iliyotolewa na mkurugenzi wa michezo wa FC Bayern Munich Hasan Salihamidzic.

“Franck amekubali kusaini mkataba mpya baada ya kuafikiana na uongozi, tunaamini kuendelea kuwepo hapa klabuni kwa msimu mmoja zaidi, kutaleta changamoto katika kikosi chetu ambacho kwa msimu ujao tumedhamiria kifike mbali zaidi, tofauti na ilivyokua msimu huu.”

Tangu mwaka 2007 Ribery ameshaifungia FC Bayern Munich mabao 80 katika michezo 247 aliyocheza.

Young Africans yawaomba radhi Sport Pesa
Putin aapishwa urais Russia