Kocha aliyeiwezesha Ivory Coast kumaliza nafasi ya pili kwenye fainali za Afrika (AFCON 2012) Francois Zahoui, ametangazwa kuwa mkuu wa benchi la ufundi la timu ya taifa ya Jamuhuri ya Afrika ya kati.

Hatua ya kutangazwa kwa kocha huyo mwenye umri wa miaka 57, imekuja juma moja baada ya kujiuzulu kukinoa kikosi cha Niger, alichokitumikia kwa miaka minne iliyopita.

“Ninathibitisha François Zahoui ndio kocha mkuu wa kikosi cha Les Fauves” alitangaza Rais wa shirikisho la soka Afrika ya kati, katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika mjini Bangui.

“Atalipwa mshahara wake wote na shirikisho la soka kuelekea michezo yetu miwili ya kuwania kufuzu AFCON 2021 dhidi ya Burundi na Mauritania, kabla ya kulikabidhi jukumu la malipo ya mshahara kwa serikali yetu,”

“Tunaamini uwezo wake wa ufundishaji utaleta tija kwenye kikosi chetu, ili kifanye vizuri katika michezo ya kuwania kufuzu AFCON 2021.”

Zahoui anachukua nafasi ya kocha kutoka Hispania Raoul Savoy, ambaye alijiuzulu mwezi Machi, baada ya kushindwa mtihani wa kuiwezesha Jamuhuri ya Afrika ya Kati kutinga katika fainali za AFCON 2019, zilizofanyika Misri miezi mitatu iliopita.

Kikosi cha Jamuhuri ya Afrika ya kati, kitaanza kampeni ya kuwania kufuzu AFCON 2021 mwezi Novemba, kwa kukabiliana na Burundi na Mauritania, kisha itapambana na mabingwa wa zamani wa Afrika, Morocco baadae mwaka 2020.

Video: RC Kagera atimba kambini kwa timu ya Kagera Sugar na kutoa maelekezo mazito
Tetesi za soka: Zaha kuihama Crystal Palace mwakani