Kiungo mpya wa Mashetani Wekundu (Manchester United) Frederico Rodrigues de Paula Santos “Fred” ameibua hofu kwenye kambi ya timu ya taifa ya Brazil, baada ya kuumia akiwa mazoezini.

Fred aliejiunga na Manchester United kwa ada ya Pauni milioni 52 mwanzoni mwa juma hili akitokea Shakhtar Donetsk, amepatwa na majeraha ya goti baada ya kugongana na kiungo wa Real Madrid Casemiro.

Wawili hao waligongana wakati wakigombea mpira, na kwa bahati mbaya Fred alionekana kuumia zaidi kuliko mwenzake.

Hata hivyo madaktari wa Brazil, walionyesha jitihada za kumpatia huduma ya kwanza kiungo huyo, na alipata ahuweni japo hakuendelea na mazoezi.

Daktari Rodrigo Lasmar, alizungumza na vyombo vya habari mara baada ya mzoezi ya timu hiyo, na kusema wataendelea kumpatia matibabu Fred na huenda ndani ya saa 24 akawa na ahuweni.

“Fred amepatwa na majeraha ya goti la mguu wake wa kulia, tunaendelea kumpatia matibabu, ninaamini saa 24 zijazo atakua na ahuweni, hivyo tuendelee kusubri.

“Nina matarajio makubwa atakua sawa kabla ya fainali za kombe la dunia, tumejiridhisha hakupata maumivu makali sana, japo ameumia.” Alisema Lasmar

Kikosi cha Brazil kimeweka kambi jijini London, na kinafanya mazoezi kwenye uwanja wa mazoezi wa klabu ya Tottenham uitwao Enfield, kaskazini mwa jijini humo.

Baadae hii leo timu ya taifa ya Brazil inatarajiwa kuondoka jijini humo na kuelekea Vienna, Austria kwa ajili ya mchezo wa mwisho wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya wenyeji utakaochezwa siku ya jumapili.

Urusi 2018: Nani atabeba Kombe? Tuimulike Korea Kusini
Video: Nyaraka za Maaskofu kaa la moto kila kona, Maisha ya kigogo IPTL hatarini

Comments

comments