Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi (Saa 72) iliyokutana jana Januari 4, 2018, imeipa Friends Rangers ushindi wa pointi tatu na mabao matatu baada ya Mvuvumwa kuchezesha wachezaji ambao hawajasajiliwa (non qualified) katika mechi ya Kundi A Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kati ya timu hizo iliyochezwa Oktoba 29, 2017. Mvuvumwa ilishinda mechi hiyo mabao 4-1.

Uamuzi huo dhidi ya Mvuvumwa umefanywa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(18) na 42(20) za Ligi Daraja la Kwanza. Nayo Friends Rangers imepewa ushindi kwa kuzingatia Kanuni ya 14(37) na ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Taratibu za Mchezo.  

Vilevile viongozi wa Mvuvumwa waliohusika kughushi leseni zilizotumiwa na wachezaji hao ambao hawakusajiliwa watafikishwa kwenye Kamati ya Maadili ya TFF kwa ajili ya hatua zaidi.

MALALAMIKO YA ALLIANCE SCHOOLS

Kamati imepitia malalamiko ya Alliance Schools kupinga uchezeshaji wa Mwamuzi wa mechi yao dhidi ya Dodoma FC iliyofanyika Desemba 30, 2017 Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.

Baada ya kupitia hoja zote, Kamati haikukubaliana na malalamiko hayo kwa vile hayakuwa na vielelezo wala kanuni za kuyathibitisha. Pia kwa suala la muda, Kamati imejiridhisha kuwa kazi ya kutunza muda ni ya Mwamuzi.

JKT Ruvu yabadilisha jina
Maamuzi kamati ya uendeshaji na usimamizi wa ligi – Ligi daraja la pili