Mmiliki wa Studio za G. Records ambazo zilitambulisha na kuwapa mafanikio wasanii wengi nchini wanaofanya vizuri hivi sasa, ameeleza namna ambavyo aliwahi kukwazwa kwa kiwango kikubwa na Mr. Blue na Ebby Skillz.

Akiongea hivi karibuni katika kipindi cha Mkasi kinachorushwa na Channel 5, G- Lover alisema kuwa moja kati ya vitu vilivyomkera katika kusimamia kazi ya muziki ni pale Mr. Blue na Ebby Skillz kwa nyakati tofauti walipoamua kuachana na label ya studio hiyo na kumzushia kuwa alikuwa anawahujumu kimapato (mwanzoni mwa miaka ya 2000).

G-Lover (kulia) akiwa na Ali Kiba

G-Lover (kulia) akiwa na Ali Kiba ambaye pia alitamtambulisha kwenye ulimwengu wa Muziki

Alisema kuwa alitumia kiasi kikubwa cha fedha kuwatengeneza wasanii hao lakini waliamua kuondoka hata kabla hajaanza kurudisha fedha zao.

G-Lover alidai kuwa ingawa alikuwa akifahamu kuwa anahujumiwa na wasanii hao lakini aliendelea kuwasaidia, kilichomuumiza ni namna walivyokuwa wakiiacha lebo yake.

Akitoa mfano wa Mr. Blue ambaye alianzia G-Records, alisema kuwa aliondoka ghafla wakati ambapo hakutegemea ingawa alikuwa amemsainisha mkataba.

“Kilichonighafirisha ni kwamba, ghafla tu anasema ‘eeh bana mimi natoka’. Nikapigiwa simu tu na Gardner kuwa bwana mimi namchukua dogo kwenye recording label yangu. nikamwambia ‘fine, lakini mimi nimeshamsainisha mkataba. Yaani katika wasanii wote ni Blue peke yake ambaye nilikuwa nimemsainisha mkataba. Nikamwambia haina tatizo. Lakini msaidie kama mimi nilivyotaka kumsaidia,” alisema G-Lover.

Kadhalika, mdau huyo mkubwa wa muziki wa Bongo Flava alieleza kuwa alikerwa zaidi na uamuzi uliochukuliwa na Ebby Skillz akiongozwa na Mr. Blue kumpaka tope kwenye mahojiano na Clouds Fm mwanzoni mwa miaka ya 2000.

“Msanii mwingine ambaye ilikuwa tatizo ambalo sikutegemea ni Ebby Skillz. Ebby Skillz nilimsikia kwenye interview redioni, ilikuwa Clouds Fm, nikaambiwa kwamba kapelekwa na Mr. Blue. Nikaambiwa ‘hebu sikiliza’.  Mimi sikusikiliza lakini kuna mtu ambaye alisikiliza akanirekodia.

“The way ambavyo aliongea kwamba anaibiwa… alikuja redioni kusema kwamba mimi katika mauzo yangu ya albam naibiwa na kwamba naona sipati kile ambacho napaswa kukipata. Ni kitu ambacho hata mama yangu mzazi ambaye ni marehemu alisikia,” alisimulia.

G-Lover alieleza kuwa kitendo cha jina lake halisi kutajwa kama mtu aliyemuibia Ebby Skillz kilimkwaza mama yake ambaye aliona jina la ukoo wake linachafuliwa. Alisema mama yake alimuita na baada ya mazungumzo ya kina alimtaka aachane na kazi ya muziki.

“Nilimwambia mimi hii kazi siwezi kuacha. Wengine hawajielewi ni utoto. So mama akawa kama ana kinyongo. Ni bora kabla hajafariki, Ebby Skillz aliweza kwenda kumuomba msamaha,” G-Lover alisimulia.

Video Mpya: Mwana FA - Asanteni Kwa Kuja
Dylan Kerr: Mnyama Simba Yu Tayari Kuwinda