Aliyekua mshambuliaji wa timu ya taifa ya Argentina na klabu ya AS Roma ya nchini Italia, Gabriel Batistuta amenyanyua sauti ya kumkingia kifua gwiji wa klabu hiyo Francesco Totti kwa kutaka asainishwe mkataba mpya.

Batistuta, ambaye pia alizitumikia klabu za Fiorentina na Inter Milan zote za nchini Italia, amenyanyua sauti ya utetezi dhidi ya Totti, kwa kuamini bado mshambuliaji huyo mwenye historia ya kipekee huko Stadio Olympico ana nafasi ya kuendelea kucheza soka.

Amesema mtu kwa Totti, anastahili kuendelea kubaki klabuni hapo kutokana na uzoefu mkubwa alioupata tangu mwaka 1989 aliposajili na kuingizwa katika timu ya vijana ya AS Roma.

Amesema kuwa na mtu kama huyo, pia kutasaidia kuwahamasisha wachezaji wengine wenye umri mdogo kucheza kwa mapenzi kama ilivyo kwa Totti, na wakati mwingine watajiona kama mashujaa kutokana na kuwa pamoja na mkongwe huyo.

Hata hivyo wakati Batitsuta akitoa utetezi huo, tayari uongozi wa AS Roma umeshamuwekea mezani mkataba wa mwaka mmoja, mshambuliaji huyo na kinachoendelea sasa ni kusubiri jibu lake kama atakubali kubaki ama kuchukua maamuzi mengine tofauti.

Totti alipandishwa katika kikosi cha AR Roma cha wakubwa mwaka 1992 na hajawahi kuhama klabuni hapo tangu kipindi hicho mpaka hivi sasa, ambapo tayari ameshacheza michezo 601 na kufanikiwa kufunga mabao 248.

Mapendekezo Ya Jackson Mayanja Yaiweka Simba Njia Panda
Chelsea Kumrejesha Romelu Lukaku Stamford Bridge