Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo ameagiza madiwani wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Arusha kulipwa shilingi 10,000 tu kwa kila kikao watakachohudhuria na sio vinginevyo.

Aidha, Gambo ameweka masharti kuwa kiasi hicho cha fedha kitalipwa kwa Baraza hilo linaloongozwa na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) pale tu ambapo kikao husika kitakamalizika na kwamba endapo kikao hakitamalizika hawatalipwa posho hiyo.

Gambo alitoa agizo hilo katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa huo (RCC) na kuungwa mkono na Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mjini, Gabriel Daqaro ambao kwa pamoja wamemsisitiza Mkurugenzi wa Jiji hilo, Athumani Kihamia kuhakikishia anayasimamia ipasavyo maagizo hayo.

Maagizo hayo yametiliwa msisitizo wakati kukiwa na msuguano mkali kuhusu kiwango cha posho wanacholipwa madiwani hao, baada ya Halmashauri hiyo kubadili kiwango hicho kilichopangwa na Baraza la Madiwani mwaka 2008 wakati CCM ilipokuwa ikiongoza baraza hilo.

Chadema waliiomba Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuingilia kati na kutoa muongozo wa posho zinazopaswa kulipwa kwa madiwani nchi nzima ili kuwe na uwiano sawa kwa wawakilishi hao.

Al-shabab wateka eneo Somalia baada ya Ethiopia kuondoa majeshi yao
Madiwani CUF wachapana ngumi kwenye kikao Tanga