Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo amewaonya wale wote wanaoingiza masuala ya siasa kwa kila jambo ambalo Serikali inalifanya kwaajili ya kuwatumikia wananchi na kuwapunguzia kero.

Ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa sensa ya watu, makazi na mifugo katika Kata ya Ngorongoro ambayo kwa sehemu kubwa imo ndani ya Hifadhi ya Mamlaka ya Ngorongoro ili kuweza kutoa huduma stahiki.

“Nyinyi wenyewe ni mashahidi wa namna ambavyo Hifadhi hii ya Mamlaka ya Ngorongoro inavyojitoa katika kuboresha maisha yenu, lengo la sensa hii ni kujua ni wakazi kiasi gani na mifugo kiasi gani iko eneo hili kwani kuna baadhi watu ambao sio wakazi halali wa eneo hili wamekuja na mifugo hali ambayo ina hatarisha ustawi wa hifadhi yetu,” amesema Gambo.

Naye Mkuu wa wilaya ya Ngorongoro, Rashid Mfaume amewataka wananchi wa tarafa hiyo kuendelea kuwapa wataalamu hao ushirikiano kwani zoezi hilo lina manufaa makubwa kwao, na pia baada ya zoezi hili wajiandae kwa zoezi la uwekaji alama mifugo ambalo litasimamiwa na wanakijiji wenyewe ili kuwaondoa hofu wananchi hao.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa takwimu za Uchumi toka Ofisi ya Takwimu ya Taifa, Joy Sawe amesema kuwa lengo ni kujua kiasi cha shughuli za kibinaadamu katika eneo hilo ili Serikali iweze kupanga mipango yake ya kiuchumi kwa usahihi.

Hata hivyo, Gambo amewaonya wale wote ambao wanaweka siasa katika kila jambo, ambapo Serikali imeweka mkakati mkubwa wa kuweza kuhakikisha wananchi wanaondolewa kero mbalimbali.

 

Marry Majaliwa awafunda wanafunzi wa kike nchini
Video: Rich Mavoko ampa shavu Fid Q