Mlinda mlango wa klabu ya Stoke City Jack Butland anatarajiwa kujumuishwa katika kikosi cha kwanza cha England, ambacho kitashuka dimbani kucheza mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Italia baadae hii leo.

Kocha mkuu wa kikosi cha England Gareth Southgate amethibitisha mbele ya waandishi wa habari kuhusu mpango huo, ambao utamsaidia mlinda mlango huyo chaguo la pili baada ya Joe Hart.

Katika mchezo wa mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya Uholanzi, Butland alikua benchi, na langoni mwa England alikuwepo Joe Hart ambaye alifanikisha kulinda ushindi wa bao moja kwa sifuri.

Kwa mara ya kwanza Butland alikaa langoni mwa England wakati wa mchezo dhidi Italia mwaka 2012, na mpaka sasa ameshaitumikia The Three Lion katika michezo mitano. Katika fainali za mataifa ya Ulaya alilazimika kuondolewa kikosini kufuatia majereha ya kifundo cha mguu.

Mlinda mlango huyo mwenye umri wa miaka 25, ameshacheza michezo 28 ya ligi kuu ya soka nchini England msimu huu wa 2017/18 akiwa na klabu yake ya Stoke City, huku akiwa na rekodi ya kutoruhusu kufungwa (Clean Sheet) katika michezo mitano, na amekubali kufungwa mabao 51.

Southgate amesema anaamini Butland ataonyesha uwezo mkubwa kutokana na kutambua uwezo wake anapokua langoni mwa klabu ya Stoke City, huku akisisitiza katika michezo mingine ya kirafiki atatoa nafasi kama hiyo kwa mlinda mlango chipukizi wa klabu ya Everton Jordan Pickford.

“Pickford huenda akapata nafasi ya kucheza katika siku za usoni, lakini itategemea na kiwango chake pindi atakaporeja katika klabu yake, jukumu langu ni kumpa nafasi kila mchezaji ili kuonyesha uwezo wa kuisaidia England,”

“Mipango iliopo hivi sasa ni kujenga uzoefu kwa kila mchezaji ili tukielekea katika fainali za kombe la dunia kusiwe na jambo geni katika ushindani tunaoutarajia.” Amesema Southgate

Katika mchezo wa hii leo England watakua wenyeji katika uwanja wa Wembley.

Marekani yawafukuza Wanadiplomasia 60 wa Urusi
Arsenal yamuongezea mkataba kiungo Mohamed Elneny.