Kocha wa muda wa timu ya taifa ya Uingereza Gareth Southgate, amechukua maamuzi magumu ya kumtema nahodha na mshambuliaji kikosi cha timu hiyo Wayne Rooney kuelekea katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia za mwaka 2018 dhidi Slovenia.

Rooney bado yupo katika wakati mgumu wa kuuthibitishia umma wa mashabiki wa soka duniani kuhusu uwezo wake kisoka, na inadaiwa kiwango chake kimeporomoka maradufu tofauti na ilivyokua miaka ya nyuma.

Southgate anadaiwa kuchukua maamuzi ya kumuweka pembeni mshambuliaji huyo, kutokana na kutoridhishwa na uwajibikaji wake wakati wa mchezo wa mwishoni mwa juma lililopita, ambapo Uingereza ilicheza dhidi ya Malta na kupata ushindi wa mabao mawili kwa sifuri.

Kuondolewa kwa Rooney kunaacha maswali mengi kwa mashabiki wa soka, kuhusu jukumu la unahodha ambalo limeanza kuchukua nafasi baina ya wachezaji wawili ambao ni kiungo wa Liverpool Henderson pamoja na beki wa Chelsea Gary Cahill.

Hata hivyo suala la Rooney liliwahi kuzungumzwa makocha waliotangulia Roy Hodgson pamoja na Sam Allardyce, ambapo walinukuliwa na vyombo vya habari wakisema kuhusu uwezo wa mshambuliaji huyo wa Man Utd kwa kusema umekua ukishuka siku hadi siku.

Maamuzi ya kuachwa kwa Rooney yamechukuliwa na Southgate huku rekodi yake ikiwa inaridhisha katika upande wa timu ya taifa ambapo mpaka sasa ameshaitumikia katika michezo 117 na kufunga mabao 53.

Video: Kipaumbele cha Serikali kwa sasa ni uendelezaji Makao Makuu Dodoma - Majaliwa.
Young Africans Kucheza Shamba La Bibi