Kocha mkuu wa timu ya taifa ya England Gareth Southgate anatarajiwa kusaini mkataba mpya wa kuendelea kuinoa timu hiyo, ambao utamuwezesha kuwa mkuu wa benchi la ufundi hadi mwaka 2022.

Southgate mwenye umri wa miaka 48, anatarajiwa kukutana na uongozi wa chama cha soka nchini England (FA) leo Al-khamis, katika kikao cha mwisho, ambacho kitaambatana na taratibu za kusaini mkataba mpya.

Mkataba wa sasa wa kocha huyo, unatarajiwa kufikia kikomo mwaka 2020, lakini hatua ya kuiongoza vyema England katika fainali za kombe la dunia na kufika nusu fainali kwa mara ya kwanza kwenye fainali za kombe la dunia baada ya miaka 28, imempa nafasi nyingine ya kuaminiwa na viongozi wa FA, sambamba na wadau wa soka.

Taarifa kutoka ndani ya FA zinaeleza kuwa, kocha huyo tayari ameshakubali baadhi ya vipengele vilivyopo kwenye mkataba mpya, na atakua akilipwa mshahara wa Pauni milioni 3 kwa mwaka.

Kuelekea mchezo ujao wa michuano ya ligi ya mataifa ya Ulaya (UEFA Nations League) dhidi ya Croatia Oktoba 12, Southgate atakua yupo ndani ya mkataba mpya wa kazi yake.

Southgate alianza kukinoa kikosi cha England Septemba 2016, kama kocha wa muda, baada ya kujiuzulu kwa kocha Sam Allardyce, na mwezi Novemba mwaka huo alisaini mkataba rasmi, na kutambulika kama kocha mkuu.

Beki huyo wa zamani wa klabu za Aston Villa na Middlesbrough aliiwezesha England kufuzu fainali za kombe la dunia, na kuifikisha hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo iliyochezw anchini Urusi, na kutolewa na Croatia kwa kufungwa mabao mawili kwa moja.

Taifa Stars itakayoikabili Cape Verde yatajwa
Maua Sama: Ngumu kusahau, zilikuwa siku ngumu katika maisha yangu

Comments

comments