Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni wa kampuni ya Simba Motors, Jitesh Ladwa amesema wanampango wa kujenga kiwanda cha kuunganisha magari aina ya pick-up ambacho kitaanza kuzalisha magari kabla ya Desemba 30, mwaka huu.

Ametoa ahadi hiyo leo Oktoba 10, 2016 mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika mazungumzo yaliyofanyika ofisini kwake Magogoni, jijini Dar es Salaam.

Ladwa amesema wameamua kuunda magari aina ya pick-up kwa sababu ya mahitaji makubwa yaliyopo nchini. amesema takwimu zinaonyesha kuwa, kwa mwaka Tanzania inanunua magari ya aina hiyo zaidi ya 4,000. Katika nchi za SADC mahitaji ni pick-up 35,000 kwa mwaka. “Tutaanza na mtaji wa dola za Marekani milioni 200 na tumeomba ekari 200 katika eneo la EPZ,” amesema.

Amesema watahitaji eneo kubwa zaidi. eneo la kiwanda cha kuunganisha magari peke yake linahitaji ekari 50, yadi za kupaki magari, eneo la viwanda vingine, eneo la kushusha na kupakia makontena yatakayokuwa yakisafirishwa kwenda nchi jirani.

Mradi huo wa majaribio, utaanza kwa kutengeneza magari 20 kila mwezi na kwamba kazi ya utengenezaji magari itaongezeka na kufikia 1,000 na baadaye 5,000 kwa mwaka. “Tunataraji gari la kwanza litazinduliwa kabla ya Krismasi, mwaka huu,” Ladwa.

Ladwa amesema uundaji wa magari hayo aina ya Foton-Tunland utafanyika kwa ubia baina ya kampuni yao, SUMA-JKT na kampuni Foton International ya China kwa kutumia teknolojia ya Kichina na kwamba magari hayo yanayotumia 4-Wheel Drive, yana uwezo wa kupita kwenye barabara za aina zote.

Naye Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Kampuni hiyo, Aatish Ladwa, amesema mradi utakapoanza, mbali ya kutoa ajira kwa Watanzania, utawezesha pia kujengwa kwa viwanda vingine vitakavyotengeneza matairi ya magari, vioo, taa, bumpers, viti na filters.

Amesema tunataraji kujenga uwezo wa wahandisi wazawa, uhamishaji wa ujuzi kwa mafundi wa Kitanzania (technology transfer), kupunguza bei kwa mlaji wa mwisho, kupunguza gharama za uzalishaji, kutekeleza azma ya Serikali ya kuifanya Tanzania kuwa ni nchi ya viwanda, kuongeza ajira kwa wanajeshi, na kuwezesha upatikanaji wa vipuri vya magari kwa urahisi na kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi.

Wafanyakazi 1,500 watapata ajira katika kiwanda hicho kwa kuanzia, ambao watakuwemo mafundi na watoa huduma mbalimbali, lakini katika kipindi cha miaka mitatu hadi mitano ajira zitaongezeka zaidi na kufikia wafanyakazi wengine 5,000 wakati uzalishaji ukiwa umepamba moto.

Baada ya kulikagua gari la mfano aina ya Foton-Tunland, Waziri Mkuu amesema anawakaribisha kwenye uwekezaji huo hasa ikizingatiwa kuwa magari hayo yana uwezo wa kupita kwenye maeneo ya vijijini ambako barabara zake siyo nzuri.

Majaliwa amesema ofisi za Serikali zinayahitaji zaidi magari hayo, hospitali za wilayani nazo pia zinayahitaji ili yaweze kutoa huduma za chanjo kwa watoto, huduma za UKIMWI, kampeni za kupambana na malaria, na huduma kwa mama wajawazito huko vijijini.

 

Ali Kiba aituhumu timu ya Diamond kwa ‘kumkanyagia waya’ show yake na Chris Brown
Lionel Messi Kuwakabili Deportivo La Coruna