Meneja wa klabu ya AC Milan Gennaro Gattuso ameendelea kuwa katika hali ya sintofahamu, kuhusu uwezekano wa usajili wa mkopo wa mshambuliaji kutoka nchini Sweden Zlatan Ibrahimovic, akitokea LA Galaxy Ya Marekani.

Gatuso amekua katika hali hiyo kila anapooulizwa na waandishi wa habari kuhusu ukweli wa usajili wa mshambuliaji huyo ambaye aliwahi kupita klabuni hapo kuanzia mwaka 2010 hadi 2012 na baadae kutimkia kwa mabingwa wa soka nchini UfaransaPSG.

Kwa mara nyingine meneja huyo aliulizwa swali hilo usiku wa kuamkia leo mara baada ya mchezo wa ligi ya Italia dhidi ya SS Lazio uliomalizika kwa sare ya bao moja kwa moja, na aliendelea kuwa katika hali ya kushindwa kutoa jibu sahihi.

Alichojibu mchezaji huyo wa zamani wa AC Milan ni kwamba, bado anaendelea kufikiria namna ya kuisaidia klabu yake, na utakapofika wakati wa usajili ataangalia kama kutakua na uwezekano wa kufanya maboresho.

“Tutaangalia wakati utakapofika, kwa sasa ninafikiria namna ya kuisaidia timu ili ipate matokeo mazuri katika michezo inayotukabili.”

“Sioni sababu ya kuanza kujibu maswali ambayo majibu yake yatapatiwa ufumbuzi mwezi mmoja baadae, suala la Ibrahimovic sitaki kulijibu kwa sasa.”

Matokeo ya sare ya bao moja kwa moja yaliyopatikana dhidi ya SS Lazio yanaendelea kuiweka AC Milan kwenye mazingira ya kuendelea kupambana ili kufikia lengo la kutwaa ubingwa mwishoni mwa msimu huu.

Mpaka sasa klabu hiyo ya mjini Milan inashika nafasi ya tano kwenye msimamo wa Serie A kwa kuwa na alama 22, ikitanguliwa na SS Lazio wenye alama 23, Inter Milan alama 28, SSC Napoli alama 29 na Juventus wakiendelea kuwa kileleni kwa kumiliki alama 37.

Takukuru yamburuza mahakamani mtumishi wa DAWASA
Serikali yazindua Viza na vibali vya ukaazi vya kielektroniki