Uongozi wa klabu ya AC Milan umeafiki kumuongezea mkataba meneja Gennaro Ivan Gattuso, baada ya kupendezwa na kazi yake tangu alipokabidhiwa jukumu la kuwa mkuu wa benchi la ufundi klabuni hapo mwezi Novemba mwaka jana.

Uongozi wa AC Milan umeafiki jambo hilo kwa kumsainisha mkataba mkataba wa miaka mitatu gwiji huyo wa zamani wa klabu hiyo ambao utamuweka madarakani hadi mwaka 2021.

Gattuso ambaye hakuwahi kufundisha klabu yoyote ya ligi daraja la kwanza nchini Italia (Serie A), alipewa majukumu ya kuwa meneja wa muda, baada ya kutimuliwa kwa Vincenzo Montella, kutokana na hali kumuendea kombo.

Kwa kipindi cha miezi kadhaa ambacho Gattuso amekaa madarakani kama mkuu wa benchi la ufundi, ameonyesha mabadiliko makubwa katika kikosi cha AC Milan na kufanikiwa kuiwezesha timu hiyo kucheza mchezo wa fainali wa michuano ya kombe la Italia (Copa Italia) dhidi ya Juventus.

Mchezo huo wa fainali umepangwa kuchezwa mwezi ujao, na mpaka sasa watabiri wa masuala ya soka wanashindwa kutoa mitazamo yao kutokanana kuimarika kwa kikosi cha AC Milan.

Hata hivyo Gattuso hakuanza vizuri majukumu yake klabuni hapo, kwani alifanikiwa kushinda mchezo mmoja miongoni mwa michezo mitano ya mwishoni mwa mwaka 2017, lakini tangu mwaka huu 2018 ulipoanza amekua na muendelezo mzuri wa matokeo, na mpaka sasa ameshinda mara nane katika michezo 11.

“Uongozi umeamua kumsaninisha mkataba mpya Gattuso, umeridhishwa na kazi yake nzuri na unaamini katika kipindi cha miaka mitatu cha mkataba wake kutakua na mabadiliko makubwa kikosini,” Imeeleza taarifa iliyotolewana AC Milan.

“Jambo kubwa ni kuendelea kumuonyesha ushirikiano wa kutosha, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea mwishoni mwa msimu huu, na utakapofika wakati wa usajili tutajitahidi kufanya linalowezekana ili kumuwezesha kuwa na kikosi imara kwa ajili ya msimu ujao.”

Kwa upande wa Gattuso ametoa shukurani zake kwa viongozi wa AC Milan pamoja na kwa wachezaji wake, ambao amekiri wamekua siri ya jambo kubwa na la msingi alilolifikia la kusiani mkataba wa miaka mitatu.

“Ninatarajia tutaendelea kupeana ushirikiano ili kufikia lengo linalokusudiwa na viongozi wetu, kila mmoja anahitaji kuiona AC Milan ikipiga hatua, na sitiweza pekee yangu, bali kinachohitajika ni ushirikiano katika kila hatua.” Amesema Gattuso.

Gattuso aliitumikia klabu ya AC Milan kwa misimu 12mfululizo kama mchezaji, na alipata mafanikio ya kutwaa ubingwa wa ligi ya Italia (Serie A) mara mbili, Ligi ya mabingwa barani Ulaya mara mbili, pamoja na ubingwa wa klabu bingwa duniani mara moja.

Alianza shughuli za ukocha akiwa na klabu ya Sion ya nchini Uswiz, kisha akarejea nchini kwao Italia kufundisha klabu ya ligi daraja la pili (Serie B) kupitia klabu ya Palermo, na baadae alitimkia nchini Ugiriki kwenye klabu ya OFI.

Juergen Klopp: Sitaki kumuharakisha Mo Salah
Rufaa ya Wambura yagonga mwamba.