Klabu ya Zesco United ya Zambia imeharibu rekodi yake ya kutopoteza michezo 25 ya ugenini katika Ligi Kuu ya nchini humo baada ya kukubali kipigo cha bao moja kwa sifuri kutoka kwa Nkwazi.

Bao la Mwila Kabwe katika uwanja wa Edwin Imboila lilimaliza rekodi hio nzuri ya kocha George Lwandamina ambaye anatarajiwa kuwa kocha mpya wa Yanga.

Zesco ilikuwa haijapoteza mchezo ugenini tangu Novemba 2014 ilipofungwa mabao mawili kwa sifuri na Nakambala Leopards iliyokuwa ikifundishwa na kocha wa zamani wa Simba, Patrick Phiri.

Lwandamina aliliongoza benchi la ufundi la Zesco ikiwa ni siku moja tu tangu arejee Zambia akitoka Dar kwenye mazungumzo na uongozi wa Yanga.

Msimu wa Zambia umebakiza michezo 10 tu, na matokeo hayo yanafifisha matumaini ya Zesco United kutetea ubingwa wake.

Zesco wapo nyuma kwa pointi 15 dhidi ya vinara Zanaco lakini wana michezo minne mkononi.

Chukua Hii: Mpoto ni mtoto wa 36 wa mzee Mrisho
FA Yapanga Ratiba Ya Robo Fainali EFL CUP