Aliyewahi kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Ubelgiji Georges Leekens ametangazwa kuwa mkuu wa benchi la ufundi la timu ya taifa ya Algeria.

Leekens ametangazwa kushika wadhifa huo, ikiwa ni siku mbili baada ya kupoteza kibarua cha kukinoa kikosi cha klabu ya  Lokeren ya nchini kwao Ubelgiji.

Shirikisho la soka nchini Algeria, limemtangaza kocha huyo mwenye umri wa miaka 67, kuwa mbadala wa Milovan Rajevac kutoka nchini Serbia, ambaye alishindwa kuhimili mikiki mikiki ya mchezo wa kwanza wa kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia, kwa kukubali kutoka sare dhidi ya Cameroon mwanzoni mwa mwezi huu.

Leekens, amewahi kukiongoza kikosi cha Ubelgiji mara mbili na alishafanya kazi barani Afrika akiwa na timu ya taifa ya Tunisia katika fainali za Afrika za mwaka 2015.

Kibarua chake cha kwanza akiwa na kikosi cha Algeria, atapambana na Nigeria katika mji wa Uyo, Novemba 12.

Algeria pia ni sehemu ya mataifa 16 ambayo yatashiriki fainali za Afrika za mwaka 2017 zitakazoanza mwezi Januari nchini Gabon, na imepangwa katika kundi B sambamba na Zimbabwe, Tunisia na Senegal.

Adil Rami: Unai Emery Alinishawishi Kujiunga PSG
David Moyes Kujibu Mashtaka, Hasira Zamponza