Beki wa FC Barcelona, Gerard Pique amesifia hatua ya mshambuliaji wa klabu hiyo Lionel Messi kukubali kusaini mkataba mpya akiihusisha na matarajio ya kufanya vyema msimu ujao wa ligi ya Hispania.

Messi amekubali kusaini mkataba mpya ambao utaendelea kumuweka Camp Nou hadi mwaka 2021, baada ya kukamilika kwa mazungumzo kati yake na uongozi wa Barca yaliyodumu kwa kipindi cha mwaka mmoja.

“Ni hatua nzuri kwa mchezaji bora kama Messi kukubali kusaini mkataba mpya, ninaamini hali hii imeibua hisia ya kupambana kwa kila mmoja wetu pindi tutakapoanza msimu mpya mwezi ujao,” amesema Pique.

“Zimekuwa taarifa njema kwa kila mchezaji klabuni hapa ambaye alikuwa akifuatilia mustakabali wa mazungumzo kati ya Messi na viongozi, sina budi kusema msimu ujao tutakuwa katika hali tofauti kutokana na faraja aliyotupatia mwenzetu,” aliongeza.

Alifafanua kuwa Messi atasaidia kufanya kila linalowezekana ili timu hiyo irejeshe heshima yake ya kutwaa ubingwa wa Hispania na hata Ulaya.

Pique aliyasema hayo alipokuwa katika mkutano na waandishi wa habari uliokuwa na lengo la kumtambulisha mdhamini mpya wa FC Barcelona huko nchini Japan.

Alisema kuwa uwepo wa timu hiyo nchini Japan utaendelea kudhihirisha kinachohitajika kwa msimu ujao na kwamba wanaamini mashabiki wanafuatilia hatua zote walizopitia hadi kufika nchini humo kutambulishwa kwa mdhamini mpya.

Beki huyo machachari aliwaahidi mashabiki wa klabu hiyo kuwa hawatawaangusha katika msimu ujao.

Meya wa jiji la Dar awafunda wajasiliamali
Usher Raymond ndani ya Serengeti Tanzania