Juhudi za kuiunga mkono Serikali kwa kuboresha maisha ya wazee nchini, zieendelea kupewa kipaumbele baada ya Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Dhahabu Geita (GGML), kutoa msaada wa magodoro 50 kwa Kituo cha Wazee Bukumbi kilichopo mkoani Mwanza.

Akikabidhi msaada huo, Ofisa Mwandamizi wa Mahusiano ya Jamii wa GGML, Shunashu Musa amesema lengo la msaada huo ni kuboresha makazi na hali ya maisha ya wazee wanaoishi katika kituo hicho na sehemu ya kuunga mkono jitihada za Serikali.

Amesema, baadhi ya wafanyakazi wa GGML wamekuwa wakisaidia kituo hicho kwa nyakati tofauti na kuchangia vifaa mbalimbali vya matumizi, ambapo kwa awamu hii menejimenti imeamua kuboresha vyumba vya kulala vinavyotumiwa na wazee hao wa kituo cha Bukumbi.

“Tulipokea ombi la kufikiria kusaidia kituo hiki kwa njia mbalimbali na tunafahamu kituo hiki kilianzishwa miaka mingi iliyopita, hivyo baadhi ya miundombinu na vifaa vinahitaji maboresho ndiyo maana uongozi uliamua kuchangia magodoro 50,” amebainisha Shunashu Musa.

Ameongeza kuwa, “Kama sehemu ya AngloGold Ashanti, moja ya maadili ya biashara ya GGML ni kwamba jumuiya na jamii tunakofanyia kazi lazima ziwe na maisha bora. Tunatumaini magodoro haya yataboresha maisha ya wazee zaidi ya 50 wanaoishi hapa.”

Akishukuru kwa msaada huo, Msimamizi wa Kituo cha Wazee cha Bukumbi, Jonas Tarimo amesema GGML imewasaidia wazee hao katika eneo la huduma za malazi bora na salama.

Amesema, “Hiki ndicho kituo pekee cha kuishi wazee kilichopo karibu na mikoa ya Geita na Mwanza. Tumebahatika kuungwa mkono na Mgodi wa Dhahabu wa Geita ndio maana tunaona wakazi wengi wanafurahia msaada huu.”

GGML imekuwa kinara wa uwekezaji, ikiweka vipaumbele katika miradi ya afya, elimu, maji, barabara na miradi ya maendeleo inayolenga kuboresha ustawi wa jamii na hivi karibuni ilitangazwa kuwa mshindi wa jumla wa makampuni yaliyofanya vyema katika sekta ya madini Tanzania.

Pacha wa Chris Brown 'apiga pesa ndefu'
Mchezaji Simba SC aishauri Azam FC