Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekataa kuzindua mradi wa ujenzi wa Ofisi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera kwa sababu gharama zilizotumika ni kubwa kuliko aina na idadi ya majengo yaliyopo.

“Nikiweka jiwe la msingi nitakuwa nimehalalisha majengo mengine yajengwe kwa gharama hii. Siwezi kuweka jiwe la msingi, gharama zilizotumika ni kubwa kuliko majengo yaliyopo. Simamieni ujenzi wa majengo yenu na mjenge kwa kutumia mfumo wa force account.”

“Nini kilisababisha hadi kibanda kigodo cha mlinzi kikajengwa kwa shilingi milioni saba? Kina matofali mangapi kama sio ulaji nini? hii si sahihi sijaweka jiwe la msingi wala kufungua na kile kibao kilichoandikwa jina langu kiondolewe. Serikali ipo makini katika usimamizi wa miradi na haya ni maelekezo ya Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.”

Mradi wa ujenzi huo umegharimu shilingi milioni 483.42, ambapo kibanda cha mlinzi kimegharimu shilingi milioni 7.03, uzio shilingi milioni 94.2, jengo la ofisi shilingi milioni 253.8 na stoo shilingi milioni 51.55.

Waziri Mkuu amesema Serikali inajenga majengo makubwa ya vituo vya afya ambayo ni jengo la mapokezi ya wagonjwa, maabara, chumba cha upasuaji, wodi ya mama na mtoto, nyumba ya daktari, chumba cha kuhifadhia maiti, kichomea taka na korido kwa gharama ya shilingi milioni 500.

Naye, Meneja Mwandamizi Usambazi wa TANESCO Makao Makuu, Mhandisi Nathanasias Nangali ambaye alisoma taarifa ya mradi huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, amesema mradi huo ulianza Septemba 11, 2018 na kukamilika Februari 08, 2020 kwa gharama za shilingi 483,422,328.02.

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Septemba 21, 2021
Rais Samia afanya Uteuzi