Mlinda mlango AC Milan Gianluigi Donnarumma amegoma kusaini mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia klabu hiyo ya mjini Milan nchini Italia.

Mtendaji mkuu wa AC Milan Marco Fassone, amethibitisha taarifa za kugoma kwa Donnarumma, baada ya kuwa na mazungumzo ya muda mrefu, ambayo yaliaminika huenda yangembadilisha mlinda mlango huyo mwenye umri wa miaka 18.

Donnarumma alisaini mkataba wa kukitumikia kikosi cha vijana cha AC Milan mwaka 2013, kabla ya kupandishwa kwenye kikosi cha wakubwa mwaka 2015 akiwa na umri wa miaka 16.

Akiwa kikosi cha kwanza mlinda mlango huyo alikua chaguo la kwanza, na tayari ameshacheza michezo 68 ndani ya misimu miwili.

Mkataba wa sasa wa Donnarumma utafikia kikomo mwaka 2018.

Hata hivyo hatua ya kukataa kusaini mkataba mpya bado haijaelezwa inapewa msukumo na jambo gani, japo inafahamika kwa kitendo hicho huenda kukamuweka sokoni Donnarumma, katika kipindi hiki cha majira ya kiangazi.

Donnarumma, ameshaitumikia timu ya taifa ya Italia chini ya umri wa miaka 21 mwaka 2015, na sasa ni miongoni mwa wachezaji walioitwa kwenye kikosi cha wakubwa.

Jordan Pickford Aweka Rekodi Mpya England
?Live: Yanayojiri Bungeni Dodoma leo Juni 16, 2017